Agano la Kale

Agano Jipya

Yoshua 24:22-30 Biblia Habari Njema (BHN)

22. Hapo Yoshua akawaambia, “Nyinyi wenyewe ni mashahidi wa nafsi zenu kwamba mmechagua kumtumikia Mwenyezi-Mungu.” Nao wakamjibu, “Sisi tu mashahidi.”

23. Naye akawaambia, “Basi, ondoeni miungu ya kigeni mliyo nayo, mkamfuate Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa moyo wenu wote.”

24. Nao, wakasema, “Tutamtumikia na kumtii Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.”

25. Hivyo, Yoshua akafanya agano na Waisraeli huko Shekemu, akawapa masharti na maagizo ya kufuata.

26. Yoshua akayaandika haya yote katika kitabu cha sheria ya Mungu; kisha, akachukua jiwe kubwa na kulisimika chini ya mwaloni katika hema ya Mwenyezi-Mungu.

27. Halafu akawaambia watu wote, “Jiwe hili ndilo litakalokuwa shahidi kwetu, maana limesikia maneno yote ambayo Mwenyezi-Mungu ametuambia. Kwa hiyo, litashuhudia dhidi yenu, ili msije mkamkana Mungu wenu.”

28. Halafu Yoshua akawaruhusu watu waondoke; nao wakaenda kila mmoja kwake.

29. Baada ya mambo hayo, Yoshua, mwana wa Nuni na mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, akafariki akiwa na umri wa miaka 110.

30. Nao wakamzika kwenye eneo ambalo alikuwa amegawiwa kuwa sehemu yake, huko Timnath-sera, katika milima ya Efraimu, kaskazini ya mlima wa Gaashi.

Kusoma sura kamili Yoshua 24