Agano la Kale

Agano Jipya

Yoshua 17:4-13 Biblia Habari Njema (BHN)

4. Mabinti hao wakamjia kuhani Eleazari na Yoshua, mwana wa Nuni, na viongozi wengine wakawaambia, “Mwenyezi-Mungu alimwamuru Mose atugawie na sisi sote nchi kama wagawiwavyo wanaume wa kabila letu.” Basi kufuatana na amri ya Mwenyezi-Mungu, Yoshua akawapatia sehemu yao kama alivyowapa wanaume wa kabila lao.

5. Kwa hiyo kabila la Manase liliongezewa sehemu mbili zaidi yaani nchi ya Gileadi na Bashani iliyoko upande mwingine wa mto Yordani,

6. kwa sababu binti za Manase waligawiwa sehemu zao kama walivyogawiwa wanaume wa kabila lao. (Nchi ya Gileadi walipewa wazawa wengine wa Manase).

7. Eneo la kabila la Manase lilianzia Asheri na kwenda hadi Mikmethathi mashariki ya Shekemu; halafu mpaka wao ukaendelea kusini hadi kwenye nchi ya wakazi wa En-tapua.

8. Nchi ya Tapua ilikuwa mali yake Manase, lakini mji wa Tapua, ambao ulikuwa mpakani, ulikuwa mali ya wazawa wa Efraimu.

9. Mpaka huo uliendelea hadi kijito cha Kana. Miji iliyokuwa kusini ya Kana ilikuwa ya Waefraimu hata ingawa ilikuwa katika nchi ya kabila la Manase. Halafu mpaka ukapita kaskazini ya kijito Kana na kuishia bahari ya Mediteranea.

10. Eneo la kusini lilikuwa la kabila la Efraimu na eneo la kaskazini lilikuwa la kabila la Manase, mpaka wake ukiwa bahari ya Mediteranea kwa upande wa magharibi. Kabila la Asheri lilikuwa kaskazini-magharibi ya eneo la Manase na kaskazini-mashariki lilikuwa kabila la Isakari.

11. Vilevile katika nchi ya kabila la Isakari na kabila la Asheri, kabila la Manase lilipatiwa miji ya Beth-sheani na Ibleamu pamoja na vijiji vyake, na miji ya Dori, En-dori, Taanaki na Megido pamoja na wakazi na vijiji vyake; na pia theluthi ya Nafathi.

12. Lakini wazawa wa Manase hawakuweza kuwafukuza wakazi wa miji hiyo, Wakanaani wakaendelea kuishi humo,

13. ingawa hata baada ya Waisraeli kuwa na nguvu zaidi, hawakuweza kuwafukuza ila tu waliwafanyisha kazi za kulazimishwa.

Kusoma sura kamili Yoshua 17