Agano la Kale

Agano Jipya

Yoshua 15:11-20 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Kisha ukaendelea upande wa kaskazini wa Ekroni, ukazunguka kuelekea Shikroni ambapo ulipita karibu na mlima Baala hadi Yabneeli ukaishia katika bahari ya Mediteranea.

12. Mpaka wa magharibi ulikuwa bahari ya Mediteranea. Ndivyo ilivyokuwa mipaka ya eneo walilopewa watu wa kabila la Yuda kulingana na koo zao.

13. Kalebu mwana wa Yefune, alipewa sehemu ya nchi ya Yuda kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Yoshua. Alipewa Kiriath-arba au mji wa Arba ambaye alikuwa babu wa Anaki. Mji huo sasa unaitwa Hebroni.

14. Kalebu alizifukuza kutoka mji huo koo tatu za Anaki yaani ukoo wa Sheshai, ukoo wa Ahimani na ukoo wa Talmai.

15. Kutoka Hebroni alikwenda kuwashambulia wakazi wa Debiri, mji ambao hapo awali uliitwa Kiriath-seferi.

16. Kalebu akatangaza kwamba atamwoza binti yake Aksa kwa mwanamume yeyote atakayeuteka mji wa Kiriath-seferi.

17. Basi, Othnieli, mwana wa Kenazi, nduguye Kalebu, akauteka mji huo, naye Kalebu akamwoza bintiye.

18. Katika siku yao ya harusi, Aksa alimwambia Othnieli amwombe Kalebu shamba. Aksa alikuwa amepanda punda, na alipokuwa anashuka chini, Kalebu akamwuliza, “Unataka nikupe nini?”

19. Aksa akamjibu, “Nipe zawadi; nipe sehemu yenye maji kwa kuwa huko Negebu ulikonipa ni kukavu.” Basi, Kalebu akampa chemchemi za maji zilizokuwa kwenye nyanda za juu na za chini.

20. Hii ndiyo nchi waliyopewa watu wa kabila la Yuda kulingana na koo zake.

Kusoma sura kamili Yoshua 15