Agano la Kale

Agano Jipya

Yobu 2:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Ikatokea tena siku nyingine, malaika wa Mungu walikwenda kukutana mbele ya Mwenyezi-Mungu, naye Shetani akajitokeza pia pamoja nao.

2. Mwenyezi-Mungu akamwuliza Shetani, “Umetoka wapi wewe?” Naye Shetani akamjibu Mwenyezi-Mungu, “Nimetoka kutembeatembea na kuzungukazunguka duniani.”

3. Mwenyezi-Mungu akamwambia Shetani, “Je, umemwangalia mtumishi wangu Yobu? Duniani hakuna mwingine aliye kama yeye. Yeye ni mtu mnyofu, mcha Mungu na mwenye kujiepusha na uovu. Yeye yuko imara katika unyofu wake, ingawa wewe umenichochea nimwangamize bure.”

4. Shetani akamjibu Mwenyezi-Mungu, “Ngozi kwa ngozi! Mtu hutoa kila kitu alicho nacho ili aokoe uhai wake.

5. Lakini sasa hebu nyosha mkono wako umguse mwili wake; nakuambia atakutukana waziwazi.”

6. Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia Shetani, “Haya! Waweza kumfanya utakavyo, walakini usimuue.”

7. Hapo Shetani akaondoka mbele ya Mwenyezi-Mungu, akamtesa Yobu kwa madonda mabaya tangu wayo wa mguu wake mpaka utosini mwake.

8. Yobu akatwaa kigae, akajikuna nacho na kuketi kwenye majivu.

9. Mkewe akamwambia, “Bado tu ungali ukishikilia unyofu wako? Mtukane Mungu, ufe.”

10. Yobu akamjibu mkewe, “Wewe unaongea kama wanawake wapumbavu. Tukipokea mema kutoka kwa Mungu, kwa nini tukatae kupokea pia mabaya kutoka kwake?” Katika mambo hayo yote, Yobu hakutamka neno lolote la kumkosea Mungu.

Kusoma sura kamili Yobu 2