Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 50:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Neno la Mwenyezi-Mungu alilosema kwa njia ya nabii Yeremia kuhusu nchi ya Babuloni na nchi ya Wakaldayo:

2. “Tangazeni kati ya mataifa,twekeni bendera na kutangaza,Msifiche lolote. Semeni:‘Babuloni umetekwa,Beli ameaibishwa.Merodaki amefadhaishwa;sanamu zake zimeaibishwa,vinyago vyake vimefadhaishwa.’

3. “Kwa maana, taifa kutoka kaskazini limefika kuushambulia; litaifanya nchi yake kuwa uharibifu. Hakuna atakeyeishi humo; watu na wanyama watakimbia mbali.

4. “Siku hizo na wakati huo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu, watu wa Israeli na watu wa Yuda watakusanyika pamoja na kurudi wakilia huku wananitafuta mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wao.

5. Watauliza njia ya kwenda Siyoni, huku nyuso zao zimeelekea huko, wakisema, ‘Njoni!’ Nao watajiunga na Mwenyezi-Mungu katika agano la milele ambalo kamwe halitasahauliwa.

6. “Watu wangu walikuwa kondoo waliopotea; wachungaji wao wamewapotosha, wakawageuza kuelekea milimani; walitembea toka mlima hadi kilima, wakasahau zizi lao.

7. Watu wote waliowakuta waliwaua, na maadui zao wamesema, ‘Hatuna hatia sisi’, maana hao wamemkosea Mwenyezi-Mungu aliye malisho yao ya kweli; Mwenyezi-Mungu ambaye ni tegemeo la wazee wao!

8. “Kimbieni kutoka Babuloni! Tokeni nje ya nchi ya Wakaldayo, muwe kama mabeberu mbele ya kundi.

9. Maana, mimi nitachochea mataifa makubwa kutoka nchi ya kaskazini washambulie Babuloni. Watajiandaa kuishambulia Babuloni na kuiteka. Mishale yao ni kama shujaa hodari asiyerudi mikono mitupu.

10. Nchi ya Wakaldayo itaporwa, na hao watakaoipora wataridhika. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.

11. “Enyi waporaji wa mali yangu!Japo mnafurahi na kushangilia,mnarukaruka kama mtamba wa ng'ombe anayepura nafaka,na kulia kama farasi dume,

12. nchi yenu ya kuzaliwa itaaibishwa;hiyo nchi mama yenu itafedheheshwa.Lo! Babuloni itakuwa ya mwisho kati ya mataifa,itakuwa nyika kame na jangwa.

Kusoma sura kamili Yeremia 50