Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 42:2-11 Biblia Habari Njema (BHN)

2. wakamwendea Yeremia, wakamwambia, “Tafadhali sikiliza maombi yetu na kutuombea dua kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, sisi sote tuliosalia (kwa maana tulikuwa wengi, lakini sasa tumebaki wachache tu, kama uonavyo).

3. Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, na atuoneshe njia anayotaka tuifuate, na kile anachotaka tukifanye.”

4. Yeremia akawajibu, “Vema; nimesikia. Nitamwomba Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kama mlivyonisihi; jibu lolote atakalonipa Mwenyezi-Mungu, nitawaambieni; sitawaficha chochote.”

5. Kisha, watu wakamwambia Yeremia, “Mwenyezi-Mungu na awe shahidi wa kweli na mwaminifu dhidi yetu ikiwa hatutafanya jinsi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako atakavyokuagiza utuambie.

6. Iwe ni jambo la kupendeza au la, sisi tutaitii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu ambaye tunakutuma kwake ili tufanikiwe tutakapomtii Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.”

7. Baada ya siku kumi, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yeremia.

8. Basi, Yeremia akamwita Yohanani mwana wa Karea, na makamanda wote wa majeshi pamoja na watu wote, wadogo kwa wakubwa, akawaambia,

9. “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli ambaye mlinituma kwake nipeleke maombi yenu, asema hivi:

10. Kama mtabaki katika nchi hii, basi, nitawajenga, wala sitawabomoa; nitawaotesha wala sitawangoa; kwa maana nitabadili nia kwa sababu ya maafa niliyowatenda.

11. Msimwogope mfalme wa Babuloni mnayemwogopa; naam, msimwogope hata kidogo. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Mimi niko pamoja nanyi kuwaokoeni na kuwasalimisha kutoka mikononi mwake.

Kusoma sura kamili Yeremia 42