Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 42:10-22 Biblia Habari Njema (BHN)

10. Kama mtabaki katika nchi hii, basi, nitawajenga, wala sitawabomoa; nitawaotesha wala sitawangoa; kwa maana nitabadili nia kwa sababu ya maafa niliyowatenda.

11. Msimwogope mfalme wa Babuloni mnayemwogopa; naam, msimwogope hata kidogo. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Mimi niko pamoja nanyi kuwaokoeni na kuwasalimisha kutoka mikononi mwake.

12. Nitawahurumieni na kumfanya mfalme awahurumie na kuwaacha nchini mwenu.

13. “Lakini mkisema: ‘Hatutaki kubaki katika nchi hii,’ na hivyo mkaacha kutii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu,

14. na kusema kwamba mtakwenda kukaa nchini Misri, ambako hamtaona vita wala kusikia sauti ya tarumbeta wala kukosa chakula,

15. basi, sikilizeni asemavyo Mwenyezi-Mungu enyi mabaki ya Yuda. Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema hivi: Kama mmekusudia kuingia nchini Misri na kukaa huko,

16. basi, vita mnavyoviogopa vitawakumba hukohuko Misri, na njaa mnayoihofia itawaandama vikali hadi Misri, na mtafia hukohuko.

17. Watu wote wenye nia ya kwenda kukaa Misri watakufa kwa njaa na maradhi mabaya wala hakuna hata mmoja wao atakayebaki au kunusurika kutokana na maafa nitakayowaletea.

18. “Maana mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Kama vile hasira yangu na ghadhabu yangu ilivyowapata wakazi wa Yerusalemu, ndivyo ghadhabu yangu itakavyowapata nyinyi, kama mtakwenda Misri. Mtakuwa kitu cha kutukanwa, kitisho, laana na aibu. Hamtapaona tena mahali hapa.”

19. Yeremia akawaambia watu: “Enyi Wayahudi mliosalia, Mwenyezi-Mungu aliwaambia msiende Misri. Jueni wazi kwamba leo nimewaonya kuwa

20. mmepotoka, mmeyahatarisha maisha yenu. Maana mlinituma kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mkiniambia, ‘Tuombee dua kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, na chochote Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu atakachosema, utuambie, nasi tutatekeleza.’

21. Leo mimi nimewaambieni lakini hamkutii chochote ambacho Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu amenituma niwaambie.

22. Basi, jueni hakika kwamba mahali mnapotamani kwenda kukaa mtafia hukohuko kwa vita, njaa na maradhi.”

Kusoma sura kamili Yeremia 42