Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 3:14-22 Biblia Habari Njema (BHN)

14. “Rudini, enyi watoto msio na uaminifu,maana, mimi ndimi Bwana wenu.Nitawachukua mmoja kutoka kila mji,na wawili kutoka katika kila ukoo,niwapeleke hadi mlimani Siyoni.Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.

15. “Nitawapeni wachungaji wanipendao moyoni, watakaowalisha kwa maarifa na busara.

16. Siku hizo, wakati mtakapokuwa mmeongezeka na kuwa wengi nchini, watu hawatalitajataja tena sanduku langu la agano. Hawatalifikiria kabisa, wala hawatalikumbuka tena; hawatalihitaji, wala hawataunda jingine.

17. Wakati huo, mji wa Yerusalemu utaitwa ‘Kiti cha Enzi cha Mwenyezi-Mungu’, na mataifa yote yatakusanyika humo mbele yangu. Hawatafuata tena ukaidi wa matendo yao.

18. Siku hizo, watu wa Yuda wataungana na watu wa Israeli, na wote kwa pamoja watatoka katika nchi ya kaskazini na kurudi katika nchi niliyowapa wazee wenu iwe mali yao.”

19. Mwenyezi-Mungu asema,“Israeli, mimi niliwaza,laiti ningekuweka miongoni mwa wanangu,na kukupa nchi nzuri ajabu,urithi usio na kifani kati ya mataifa yote.Nilidhani ungeniita, ‘Baba Yangu’,na kamwe usingeacha kunifuata.

20. Lakini kama mke asiye mwaminifu amwachavyo mumewe,ndivyo ulivyokosa uaminifu kwangu.Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.

21. “Kelele zasikika juu ya vilima:Waisraeli wanalia na kuomboleza,kwa kuwa wamepotoka katika njia zao,wamenisahau mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wao.

22. Rudini, enyi watoto msio na uaminifu,mimi nitaponya utovu wenu wa uaminifu.“Nanyi mwasema: ‘Tazama, sisi tunarudi kwako,maana, wewe ndiwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.

Kusoma sura kamili Yeremia 3