Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 3:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

1. “Mume akimpa talaka mkewe,naye akaondoka kwake,na kuwa mke wa mwanamume mwingine,je mume yule aweza kumrudia mwanamke huyo?Je, kufanya hivyo hakutaitia nchi unajisi mkubwa?Wewe Israeli, umefanya ukahaba na wapenzi wengi,je, sasa unataka kunirudia mimi?

2. Inua macho uvitazame vilele vya vilima!Pako wapi mahali ambapo hawajalala nawe?Uliwangoja wapenzi wako kando ya njia,kama bedui aviziavyo watu jangwani.Umeifanya nchi kuwa najisi,kwa ukahaba wako mbaya kupindukia.

3. Ndiyo maana manyunyu yamezuiliwa,na wala mvua za vuli hazijanyesha.Hata hivyo uko macho makavu kama kahaba,huna haya hata kidogo.

4. “Hivi punde tu si ulinililia ukisema:‘Wewe u baba yangu,ulinipenda tangu utoto wangu?

5. Je, utanikasirikia daima?Utachukizwa nami milele?’Israeli, hivyo ndivyo unavyosema;na kumbe umetenda uovu wote ulioweza.”

6. Wakati wa utawala wa mfalme Yosia, Mwenyezi-Mungu aliniambia hivi: “Je, umeona jinsi Israeli asiye mwaminifu alivyofanya? Aliniacha, akapanda juu ya kila kilima kirefu na kwenda chini ya kila mti wenye majani mabichi, akafanya ukahaba wake humo!

7. Mimi nilidhani kuwa baada ya kufanya yote hayo, atanirudia. Lakini wapi; hakunirudia. Yuda, dada yake mdanganyifu, alishuhudia yote hayo.

8. Zaidi ya hayo, Yuda alishuhudia kuwa nilimpa Israeli talaka kwa sababu ya ukahaba wake na kwa kukosa uaminifu kwangu. Lakini hata hivyo, Yuda, dada yake mdanganyifu, hakuogopa; naye pia alikwenda na kufanya ukahaba!

9. Na, kwa kuwa yeye aliona kuwa ukahaba ni jambo dogo sana kwake, aliitia nchi unajisi, na kufanya ukahaba kwa kuabudu mawe na miti.

10. Pamoja na hayo yote, Yuda, dada mdanganyifu wa Israeli, hakunirudia kwa moyo wote, bali kwa unafiki tu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”

Kusoma sura kamili Yeremia 3