Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 15:11-21 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Haya basi, ee Mwenyezi-Mungu, acha laana hizo nizipate kama sijakutumikia vema na kama sikukusihi kwa ajili ya maadui zangu wakati walipokuwa katika taabu na shida!

12. Je, mtu aweza kuvunja chuma, chuma kitokacho kaskazini, au shaba?

13. Mwenyezi-Mungu asema: “Nitaifanya mali yenu na hazina zenu zichukuliwe nyara tena bila kulipwa fidia yoyote kwa sababu ya dhambi zenu zote mlizotenda kila mahali nchini.

14. Nitawafanya muwatumikie maadui zenu katika nchi msiyoijua kwa sababu hasira yangu imewaka moto ambao hautazimwa milele.”

15. Nami nikasema: “Lakini wewe Mwenyezi-Mungu wajua;unikumbuke na kuja kunisaidia.Nilipizie kisasi watesi wangu.Wewe u mvumilivu, usiniache niangamie;kumbuka kuwa ninatukanwa kwa ajili yako.

16. Mara maneno yako yalipofika, niliyameza;nayo yakanifanya niwe na furaha,yakawa utamu moyoni mwangu,maana mimi najulikana kwa jina lako,ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi.

17. Sikuketi pamoja na wanaostarehe,wala sikufurahi pamoja nao.Niliketi peke yangu nimelemewa nguvu yako;kwa maana ulinijaza hasira yako.

18. Kwa nini mateso yangu hayaishi?Mbona jeraha langu haliponi,wala halitaki kutibiwa?Ama kweli umenidanganya,kama kijito cha maji ya kukaukakauka!”

19. Mwenyezi-Mungu akajibu:“Kama ukinirudia nitakurudishia hali ya kwanza,nawe utanitumikia tena.Kama ukisema maneno ya maana na sio ya upuuzi,basi utakuwa msemaji wangu.Watu watakuja kujumuika nawe,wala sio wewe utakayekwenda kwao.

20. Mbele ya watu hawa,nitakufanya ukuta imara wa shaba.Watapigana nawe,lakini hawataweza kukushinda,maana, mimi niko pamoja nawe,kukuokoa na kukukomboa.Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.

21. Nitakuokoa mikononi mwa watu waovu,na kukukomboa makuchani mwa wakatili.”

Kusoma sura kamili Yeremia 15