Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 11:4-11 Biblia Habari Njema (BHN)

4. Hili ni agano nililowapa wazee wenu nilipowatoa nchini Misri, kutoka katika tanuri la chuma. Niliwaambia wanitii na kufanya yote niliyowaamuru, na kwamba wakifanya hivyo, watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao.

5. Wakifuata masharti hayo, mimi nitatimiza ahadi niliyowapa wazee wenu, kwamba nitawapa nchi inayotiririka maziwa na asali, kama ilivyo hadi leo.” Nami nikajibu: “Na iwe hivyo, ee Mwenyezi-Mungu.”

6. Mwenyezi-Mungu akaniambia: “Tangaza masharti hayo yote katika miji ya Yuda na katika barabara za Yerusalemu. Waambie watu wayasikilize masharti ya agano hili na wayatekeleze.

7. Maana niliwaonya vikali wazee wao nilipowatoa katika nchi ya Misri, na nimeendelea kuwaonya wanitii mpaka siku hii ya leo.

8. Lakini wao hawakunitii, wala hawakunisikiliza. Badala yake, kila mmoja wao alizidi kuwa mkaidi na mwovu. Basi, niliwaadhibu kulingana na masharti ya agano hili nililowaamuru walishike, lakini hao wakakataa kulishika.”

9. Tena Mwenyezi-Mungu aliniambia: “Watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu wanafanya njama za kuniasi.

10. Wameurudia uovu wa wazee wao ambao walikataa kusikiliza maneno yangu; wameiabudu miungu mingine na kuitumikia. Watu wa Israeli na watu wa Yuda wamevunja agano nililofanya na wazee wao.

11. Kwa hiyo, sasa, mimi Mwenyezi-Mungu ninawaonya kwamba nitawaletea maafa ambayo hawataweza kuepukana nayo. Hata kama wakinililia namna gani, sitawasikiliza.

Kusoma sura kamili Yeremia 11