Agano la Kale

Agano Jipya

Walawi 7:21-36 Biblia Habari Njema (BHN)

21. Mtu yeyote anayegusa kitu chochote kilicho najisi, au kitu najisi cha mtu, au mnyama aliye najisi, au kitu chochote najisi ambacho ni chukizo, akila nyama ya sadaka ya amani aliyotolewa Mwenyezi-Mungu, mtu huyo atatengwa na watu wake.”

22. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose,

23. “Waambie Waisraeli hivi: Msile mafuta ya ng'ombe au ya kondoo au ya mbuzi.

24. Mafuta ya mnyama yoyote aliyekufa mwenyewe au ya mnyama aliyeuawa na mnyama wa porini yaweza kuwekwa kwa matumizi mengine, lakini kamwe msiyale.

25. Mtu yeyote akila mafuta ya mnyama aliyetolewa kwa Mwenyezi-Mungu kwa moto, atatengwa na watu wake.

26. Tena, kamwe msile damu yoyote ile, iwe ya ndege au ya mnyama mahali popote mnapoishi.

27. Mtu yeyote akila damu yoyote, atatengwa na watu wake.”

28. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose,

29. “Waambie watu wa Israeli hivi: Mtu yeyote akitoa sadaka ya amani, atampa Mwenyezi-Mungu sehemu ya sadaka hiyo.

30. Atamletea kwa mikono yake mwenyewe kama sadaka ya kuteketezwa kwa moto. Ataleta mafuta yake pamoja na kidari ambacho atafanya nacho ishara ya kumtolea Mwenyezi-Mungu.

31. Kuhani atayateketeza mafuta yote juu ya madhabahu, lakini kidari kitakuwa cha Aroni na wanawe makuhani.

32. Mguu wa kulia wa nyuma wa mnyama wa sadaka zenu za amani mtampa kuhani.

33. Mguu huo utakuwa mali ya kuhani aliye mzawa wa Aroni anayetoa damu ya sadaka za amani na mafuta yake.

34. Mwenyezi-Mungu amewaagiza watu wa Israeli watenge kidari hicho na mguu huo wa mnyama wa sadaka zao za amani, wampe kuhani Aroni na wazawa wake, maana sehemu hiyo wamewekewa hao makuhani milele.

35. Hiyo ndiyo sehemu iliyotengwa kwa ajili ya Aroni na wanawe kutoka katika sadaka anazotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto, tangu siku walipotawazwa kuwa makuhani wa Mwenyezi-Mungu.

36. Walipowekwa wakfu kwa kupakwa mafuta, Mwenyezi-Mungu aliamuru Waisraeli wawape sehemu hiyo ya sadaka; hiyo itakuwa daima haki yao.”

Kusoma sura kamili Walawi 7