Agano la Kale

Agano Jipya

Waamuzi 9:46-57 Biblia Habari Njema (BHN)

46. Watu wote waliokuwa katika mnara wa Shekemu waliposikia habari hizo, walikimbilia kwenye ngome ya nyumba ya mungu aliyeitwa El-berithi.

47. Abimeleki akaambiwa kuwa watu wote waliokuwa kwenye mnara wa Shekemu wamejikusanya pamoja.

48. Abimeleki na watu wake wakaenda mlimani Salmoni, akachukua shoka akakata tawi la mti na kuliweka begani mwake. Halafu akawaambia wale watu aliokuwa nao waharakishe kufanya kama alivyofanya.

49. Kila mmoja akakata tawi kama lile la Abimeleki. Wakachukua matawi yao na kuyaegemeza kwenye kuta za ngome, wakayatia moto na kuichoma ngome; watu wote wanaume na wanawake wapatao 1,000 waliokuwa katika mnara wa Shekemu wakafa.

50. Kisha Abimeleki akaenda Thebesi, akauzingira na kuuteka.

51. Lakini kulikuwa na mnara imara katikati ya mji. Basi, wakazi wote wa mji huo wanaume na wanawake wakakimbilia humo na kujifungia ndani. Wakapanda kwenye paa la mnara huo.

52. Abimeleki aliufikia mnara na kuushambulia, kisha, aliukaribia mlango wa mnara autie moto.

53. Naye mwanamke mmoja akatupa jiwe la juu la kusagia, akamponda Abimeleki kichwa.

54. Kisha Abimeleki akamwita haraka kijana wake aliyembebea silaha akamwambia, “Chukua upanga wako uniue, wasije watu wakasema kuwa niliuawa na mwanamke.” Kijana akachukua upanga wake, akamchoma na kumuua.

55. Waisraeli walipoona kwamba Abimeleki amekufa, wakaondoka na kurudi kila mmoja nyumbani kwake.

56. Hivyo ndivyo Mungu alivyomwadhibu Abimeleki kwa kosa lake dhidi ya baba yake kwa kuwaua ndugu zake sabini.

57. Vilevile Mungu aliwafanya watu wa Shekemu waadhibiwe kwa uovu wao walioufanya. Hivyo, laana ya Yothamu mwana wa Yerubaali ikawapata.

Kusoma sura kamili Waamuzi 9