Agano la Kale

Agano Jipya

Waamuzi 3:19-29 Biblia Habari Njema (BHN)

19. Lakini yeye alipofika kwenye sanamu za mawe yaliyochongwa karibu na Gilgali, alimrudia Egloni akasema, “Nina ujumbe wa siri kwako, ee mfalme.” Mfalme akawaamuru watumishi wakae kimya, nao wakatoka nje.

20. Naye Ehudi akamkaribia pale alipokaa katika chumba chake chenye baridi barazani, akamwambia “Nina ujumbe wako kutoka kwa Mungu.” Mfalme akainuka kitini mwake na kusimama.

21. Ehudi akauchomoa upanga wake kwa mkono wake wa kushoto kutoka paja lake la kulia, akamchoma nao tumboni mwake.

22. Upanga ukaingia ndani pamoja na mpini wake, mafuta yakaufunika upanga huo kwani Ehudi hakuutoa tena; ukawa umetokea kwa nyuma.

23. Kisha, Ehudi akatoka nje barazani baada ya kuifunga milango ya chumba hicho kwa ufunguo.

24. Ehudi alipoondoka, watumishi wa mfalme wakarudi. Walipoona milango yote ya chumba imefungwa, walifikiri amekwenda kujisaidia chooni humo ndani ya nyumba.

25. Wakangojea mpaka wakaanza kuwa na wasiwasi. Walipoona hafungui, wakachukua ufunguo na kufungua mlango. Wakamwona mfalme wao sakafuni, naye amekufa.

26. Walipokuwa wanangoja, Ehudi alitoroka akipitia kwenye sanamu za mawe, akaenda Seira.

27. Alipofika huko alipiga tarumbeta katika nchi ya milima ya Efraimu, nao Waisraeli wakateremka pamoja naye kutoka huko milimani naye akawatangulia.

28. Akawaambia, “Mnifuate, maana Mwenyezi-Mungu amewatia adui zenu Wamoabu mikononi mwenu.” Wakamfuata mpaka kivuko cha Yordani na kukiteka toka mikononi mwa Wamoabu, wakazuia mtu yeyote kupita.

29. Siku hiyo, wakawaua Wamoabu wapatao 10,000; watu wote wenye afya na nguvu, wala hakuna hata mmoja aliyenusurika.

Kusoma sura kamili Waamuzi 3