Agano la Kale

Agano Jipya

Waamuzi 14:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Siku moja, Samsoni aliteremka na kwenda Timna ambako alimwona msichana mmoja Mfilisti.

2. Aliporudi nyumbani akawaambia wazazi wake, “Nimemwona msichana mmoja Mfilisti huko Timna. Niozeni msichana huyo.”

3. Lakini wazazi wake wakamwambia, “Je, hakuna msichana yeyote miongoni mwa ndugu zako au kati ya watu wetu hata uende kuoa kwa Wafilisti wasiotahiriwa?” Lakini Samsoni akamwambia baba yake, “Niozeni msichana huyo, maana ananipendeza sana.”

4. Wazazi wake hawakujua kwamba huo ulikuwa mpango wa Mwenyezi-Mungu ambaye alikuwa anatafuta kisa cha kuchukua hatua dhidi ya Wafilisti. Wakati huo, Wafilisti waliwatawala Waisraeli.

5. Samsoni na wazazi wake waliondoka kwenda Timna. Walipofika huko kwenye mashamba ya mizabibu, mwanasimba mmoja akatokea akamngurumia Samsoni.

6. Basi, roho ya Mwenyezi-Mungu ikamwingia Samsoni kwa nguvu, akamrarua simba huyo kama mtu araruavyo mwanambuzi. Naye Samsoni hakuwaambia wazazi wake kisa hicho.

7. Kisha akateremka akaenda kuzungumza na yule msichana; huyo msichana alimpendeza sana Samsoni.

8. Baada ya siku chache alirudi huko Timna kumchukua huyo msichana. Alipokuwa njiani akageuka pembeni kuuona mzoga wa yule simba, na kumbe kulikuwa na nyuki ndani ya mzoga na asali.

9. Basi, akapakua asali kwa mikono yake akawa anakula huku akiendelea na safari yake. Aliporudi kwa wazazi wake, akawapa asali kidogo nao wakala. Lakini hakuwaambia kwamba alitoa asali hiyo ndani ya mzoga wa simba.

10. Baba yake akaenda nyumbani kwa yule msichana, naye Samsoni akafanya karamu huko, kama walivyofanya vijana wakati huo.

11. Wafilisti walipomwona Samsoni wakamletea vijana thelathini wakae naye.

Kusoma sura kamili Waamuzi 14