Agano la Kale

Agano Jipya

Waamuzi 1:5-17 Biblia Habari Njema (BHN)

5. Katika mji huo walimkuta mfalme Adoni-bezeki, wakapigana naye na kuwashinda Wakanaani na Waperizi.

6. Adoni-bezeki akakimbia, lakini walimfuatia, wakamkamata, wakamkata vidole gumba vya mikono na miguu.

7. Adoni-bezeki akasema, “Wafalme sabini waliokatwa vidole gumba vya mikono na miguu waliokota makombo chini ya meza yangu. Sasa Mungu amenilipa kama nilivyotenda.” Wakampeleka Yerusalemu, akafia huko.

8. Watu wa kabila la Yuda waliushambulia mji wa Yerusalemu na kuuteka. Waliwaua wakazi wake kwa mapanga na kuuteketeza mji kwa moto.

9. Baadaye, watu wa kabila la Yuda walikwenda kupigana na Wakanaani walioishi kwenye nchi ya milima, Negebu na kwenye nchi tambarare.

10. Waliwashambulia pia Wakanaani walioishi katika mji wa Hebroni ambao hapo awali uliitwa Kiriath-arba, wakashinda makabila ya Sheshai, Himani na Talmai.

11. Kutoka huko watu wa kabila la Yuda walikwenda kuushambulia mji wa Debiri; ambao hapo awali uliitwa Kiriath-seferi.

12. Kalebu akatangaza: “Mtu yeyote atakayefaulu kuuteka mji wa Kiriath-seferi, nitamwoza binti yangu Aksa.”

13. Basi, Othnieli, mwana wa Kenazi na mdogo wake Kalebu, akauteka, naye Kalebu akamtoa bintiye Aksa aolewe na Othnieli.

14. Aksa alipowasili kwa Othnieli, akamwambia Othnieli amwombe Kalebu baba yake shamba. Aksa alikuwa amepanda punda na aliposhuka chini baba yake alimwuliza, “Ungependa nikupe nini?”

15. Akamjibu, “Nipe zawadi! Naomba unipe chemchemi za maji kwani eneo ulilonipa huko Negebu ni kavu.” Kalebu akampa chemchemi za juu na za chini.

16. Wazawa wa Keni ambaye alikuwa baba mkwe wa Mose, walifuatana na watu wa kabila la Yuda kutoka Mji wa Mitende yaani mji wa Yeriko, mpaka jangwa la Yuda karibu na Aradi, wakafanya makao yao huko pamoja na watu wa Yuda.

17. Watu wa kabila la Yuda walishirikiana na ndugu zao, watu wa kabila la Simeoni, wakawashinda Wakanaani waliokaa Sefathi. Waliuangamiza kabisa mji huo na kugeuza jina lake kuwa Horma.

Kusoma sura kamili Waamuzi 1