Agano la Kale

Agano Jipya

Ruthu 2:4-18 Biblia Habari Njema (BHN)

4. Baada ya muda, Boazi alifika kutoka Bethlehemu akawasalimu wavunaji, akasema, “Mwenyezi-Mungu awe nanyi.” Nao wakamjibu, “Mwenyezi-Mungu na akubariki.”

5. Kisha Boazi akamwuliza msimamizi wa wavunaji, “Je, yule msichana ni nani?”

6. Huyo kiongozi wa wavunaji akajibu, “Ni msichana Mmoabu aliyekuja pamoja na Naomi kutoka katika nchi ya Moabu.

7. Aliniomba nimruhusu awafuate nyuma wavunaji huku akiokota masazo kati ya miganda. Basi alikuja na amefanya kazi tangu asubuhi na ni sasa tu amekwenda kupumzika kibandani.”

8. Ndipo Boazi akamwambia Ruthu, “Hebu sikiliza binti yangu. Usiende kuokota masuke mahali pengine ila katika shamba hili tu. Fuatana na wanawake hawa;

9. angalia mahali wavunapo ujiunge nao. Nimewaonya vijana hawa wasikusumbue. Na ukiona kiu, nenda kwenye mitungi na unywe maji waliyoyateka hao vijana.”

10. Hapo Ruthu akamwinamia Boazi mpaka chini kwa unyenyekevu, akamwambia, “Nimepataje kibali chako? Mbona unanihurumia na hali mimi ni mgeni tu?”

11. Lakini Boazi akamjibu, “Nimeyasikia yote uliyomfanyia mama mkwe wako tangu mumeo afariki. Ninajua jinsi ulivyowaacha wazazi wako, ukaiacha nchi yako, na jinsi ulivyokuja kuishi kati ya watu ambao hukuwajua hapo awali.

12. Mwenyezi-Mungu akujaze kwa yote uliyoyafanya. Mwenyezi-Mungu wa Israeli uliyemkimbilia akulinde chini ya mabawa yake, akupe thawabu kamilifu.”

13. Ruthu akamjibu, “Bwana, wewe umenifanyia wema mkubwa sana. Ingawa mimi si kama mmoja wa watumishi wako, nimeridhika kwa kuwa umenifariji sana na kuongea nami kwa ukarimu.”

14. Wakati wa chakula, Boazi alimkaribisha Ruthu akamwambia, “Karibu hapa, njoo ule mkate pia na uuchovye ndani ya divai.” Kwa hiyo Ruthu akaketi pamoja na wavunaji, na Boazi akampa nafaka iliyokaangwa, akala akashiba hata akabakiza.

15. Na ikawa Ruthu alipoendelea kuokota mavuno, Boazi aliwaambia wafanyakazi wake, “Mwacheni akusanye hata mahali miganda ilipo wala msimkemee.

16. Zaidi ya hapo, vuteni masuke kutoka katika matita na mumwachie aokote bila kumkaripia.”

17. Basi Ruthu aliendelea kuokota masuke mpaka jioni; na baada ya kupura hiyo shayiri alipata debe moja na zaidi.

18. Kisha akachukua mavuno hayo hadi mjini na kumwonesha mama mkwe wake kiasi alichookota. Pia alikitoa kile chakula alichobakiza baada ya kushiba, akampa.

Kusoma sura kamili Ruthu 2