Agano la Kale

Agano Jipya

Nehemia 4:12-23 Biblia Habari Njema (BHN)

12. Wayahudi waliokaa miongoni mwa adui zetu waliposikia maneno yao, walitujia mara kumi wakisema, “Watakuja toka kila mahali wanapokaa na kutushambulia.”

13. Hivyo, kwenye sehemu za chini za ukuta ambazo zilikuwa bado kumalizika, nyuma ya ukuta, katika mahali pa wazi, niliwapanga watu kulingana na jamaa zao wakiwa na mapanga, mikuki na pinde.

14. Nilipoona kuwa watu walikuwa na hofu nikawaambia wakuu, maofisa na watu wote kwa ujumla, “Msiwaogope hata kidogo. Mkumbukeni Bwana aliye Mkuu na wa kutisha, basi piganeni kwa ajili ya ndugu zenu, wana wenu, binti zenu, wake zenu na nyumba zenu.”

15. Maadui waliposikia kwamba njama zao tumezigundua na kuwa Mungu amevuruga njama hizo, ndipo sisi sote tulipourudia ukuta, kila mmoja akaendelea na kazi yake.

16. Tokea siku hiyo na kuendelea, nusu ya watumishi wangu wakawa wanaendelea na ujenzi ambapo nusu nyingine ikawa inashika ulinzi wakiwa na mikuki, ngao, pinde na mavazi ya kukinga kifua. Viongozi wetu wakawa upande wa watu wa Yuda

17. waliokuwa wanaujenga ukuta. Hata wale waliokuwa wanabeba vifaa vya ujenzi waliendelea na kazi huku mkono mmoja ukiwa na vifaa vya ujenzi na mkono mwingine silaha yake.

18. Kila mwashi alikuwa na panga lake limefungwa kiunoni mwake na huku anaendelea kujenga. Na mtu wa kupiga tarumbeta alikuwa karibu nami.

19. Nikawaambia wakuu, maofisa na watu wote kwa ujumla “Kazi ni kubwa, nayo imeenea sehemu kubwa hivi ya kwamba tumetawanyika mno juu ya ukuta kila mmoja yuko mbali na mwenzake.

20. Ukiwa mahali popote unapofanya kazi, mara utakaposikia tarumbeta, kimbilia kwetu. Mungu wetu atatupigania.”

21. Hivyo, tukaendelea kufanya kazi yetu na nusu ya watu wakishika silaha tangu mapambazuko hadi nyota zinapoonekana mbinguni.

22. Wakati huo nikawaambia watu, “Kila mwanamume na mtumishi wake atakaa mjini Yerusalemu usiku, ili tuwe na ulinzi usiku, na wakati wa mchana wataendelea na kazi.”

23. Hivyo ikawa mimi, ndugu zangu, watumishi wangu hata na walinzi waliofuatana nami, hatukuvua mavazi yetu; kila mmoja wetu akawa daima na silaha yake mkononi.

Kusoma sura kamili Nehemia 4