Agano la Kale

Agano Jipya

Nehemia 13:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Katika siku hiyo ya sherehe, kitabu cha Mose kilisomwa na ilifahamika kuwa Waamoni na Wamoabu kamwe wasiingie katika mkutano wa watu wa Mungu.

2. Maana watu wa Israeli, walipokuwa wanasafiri toka Misri, hawakuwapa chakula wala maji ya kunywa, badala yake walimkodisha Balaamu kuwalaani watu wa Israeli, lakini Mungu wetu aligeuza laana yao kuwa baraka.

3. Watu wa Israeli waliposikia sheria hiyo waliwatenga watu wa mataifa mengine.

4. Kabla ya siku ya sherehe, kuhani Eliashibu aliyekuwa ameteuliwa kuangalia vyumba vya nyumba ya Mungu wetu, na mwenye uhusiano mwema na Tobia,

5. alimruhusu Tobia kutumia chumba kikubwa ambamo hapo awali walikuwa wameweka tambiko za nafaka, ubani, vyombo, zaka za nafaka, divai, mafuta; vitu hivyo vyote Waisraeli walivyoagizwa kuwapa Walawi, waimbaji, walinda malango, na matoleo kwa makuhani.

6. Wakati mambo haya yalipokuwa yanatendeka mimi sikuwako Yerusalemu; kwani katika mwaka wa thelathini na mbili wa utawala wa mfalme Artashasta wa Babuloni, nilikuwa nimeomba likizo; nami nikaenda kutoa ripoti kwake.

7. Niliporudi Yerusalemu ndipo nikagundua uovu wa Eliashibu wa kumpa Tobia chumba katika ua wa nyumba ya Mungu.

8. Nilikasirika sana na nikavitupa nje vyombo vyote vya Tobia.

9. Niliamuru watu, nao wakatakasa vyombo hivyo, ndipo nikarudisha humo vifaa vya nyumba ya Mungu, pamoja na tambiko za nafaka na ubani.

10. Tena nikagundua kuwa Walawi hawakupewa haki zao; na matokeo yake ni kwamba Walawi na waimbaji waliokuwa wakifanya kazi hapo awali, sasa walikwisha rudia mashamba yao.

11. Nikawakemea viongozi, nikasema, “Kwa nini nyumba ya Mungu imeachwa?” Niliwakusanya pamoja na kuwarudisha kazini.

12. Kisha, watu wote wa Israeli, wakaanza tena kuleta zaka zao za nafaka, divai na mafuta kwenye ghala.

13. Nikawateua watu wafuatao kuwa watunzaji wa ghala: Kuhani Shelemia, mwandishi Sadoki na Pedaia Mlawi. Hanani, mwana wa Zakuri, mwana wa Matania akawa msaidizi wao. Walikuwa waaminifu na kazi yao ilikuwa kuwagawia ndugu zao mahitaji yao.

14. Ee, Mungu wangu, nikumbuke kwa ajili ya haya yote na usiyasahau matendo yangu mema niliyofanya kwa ajili ya nyumba yako na kwa ajili ya huduma yako.

Kusoma sura kamili Nehemia 13