Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 8:13-22 Biblia Habari Njema (BHN)

13. Noa alipokuwa na umri wa miaka 601, siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, maji yalikuwa yamekauka katika nchi. Noa akafunua kifuniko cha safina na alipotazama, akaona kwamba nchi ilikuwa imekauka.

14. Siku ya 27 ya mwezi wa pili, nchi ilikuwa imekauka kabisa.

15. Hapo, Mungu akamwambia Noa,

16. “Toka katika safina, wewe pamoja na mkeo, wanao na wake zao.

17. Toa pia viumbe wote hai wa kila aina waliokuwa pamoja nawe, ndege na wanyama na kila kiumbe kitambaacho, wapate kuzaa kwa wingi duniani, waongezeke na kuenea kila mahali duniani.”

18. Basi, Noa akatoka katika safina pamoja na wanawe na mkewe pamoja na wake za wanawe.

19. Wakatoka kufuatana na jamii zao, wanyama wote wa porini, viumbe wote watambaao, ndege wote na wanyama wote hai duniani.

20. Noa akamjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu, akatwaa mmoja katika kila aina ya wanyama walio safi na ndege walio safi, akamtolea Mungu sadaka za kuteketezwa.

21. Harufu nzuri ya tambiko hiyo ikampendeza Mwenyezi-Mungu, naye akasema moyoni mwake, “Kamwe sitailaani tena nchi kwa sababu ya binadamu; najua kwamba mawazo yake ni maovu tangu utoto wake. Wala sitaangamiza tena viumbe wote kama nilivyofanya.

22. Kadiri itakavyodumu nchi majira ya kupanda na kuvuna, ya baridi na joto, ya masika na kiangazi, usiku na mchana, hayatakoma.”

Kusoma sura kamili Mwanzo 8