Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 7:12-23 Biblia Habari Njema (BHN)

12. Mvua ikanyesha nchini siku arubaini mchana na usiku.

13. Siku hiyohiyo mvua ilipoanza kunyesha, Noa, mkewe na wanawe, Shemu, Hamu na Yafethi, pamoja na wake zao, waliingia ndani ya safina.

14. Waliingia wao wenyewe pamoja na aina zote za wanyama wa porini, wanyama wafugwao, wanyama watambaao na ndege wa kila aina.

15. Waliingia ndani ya safina pamoja na Noa wiliwawili wa kila aina ya viumbe hai.

16. Kila aina yao waliingia, dume na jike, kama Mungu alivyomwamuru Noa. Kisha, Mwenyezi-Mungu akaufunga mlango wa safina nyuma yake Noa.

17. Gharika ilidumu nchini kwa muda wa siku arubaini. Maji yakaongezeka na kuiinua safina, ikaelea juu ya ardhi.

18. Maji yakaendelea kuongezeka zaidi nchini na safina ikaelea juu yake.

19. Maji hayo yakawa mengi sana juu ya nchi, yakaifunika milima yote mirefu katika nchi.

20. Yaliongezeka hata kuifunika milima kiasi cha mita saba na nusu.

21. Viumbe wote hai katika nchi wakafa. Ndege, wanyama wa kufugwa, wanyama wa porini, makundi ya viumbe wote katika nchi kavu na wanadamu wote;

22. naam, kila kiumbe hai katika nchi kavu kilikufa.

23. Mungu akaangamiza kila kiumbe kilichokuwa hai duniani: Binadamu, wanyama, viumbe vitambaavyo na ndege wa angani. Vyote viliangamizwa duniani. Noa tu ndiye aliyesalimika na wale waliokuwa pamoja naye ndani ya safina.

Kusoma sura kamili Mwanzo 7