Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 45:16-28 Biblia Habari Njema (BHN)

16. Habari hizo zilipofika ikulu ya mfalme, kwamba ndugu za Yosefu wamekuja, zikamfurahisha sana Farao na watumishi wake.

17. Kwa hiyo, Farao akamwambia Yosefu, “Waambie ndugu zako wawapakie punda wao mizigo, warudi nchini Kanaani,

18. wamlete hapa baba yao na jamaa zao wote. Mimi nitawapa sehemu nzuri kabisa ya nchi ya Misri, ambako wataweza kufurahia matunda yote ya nchi hii.

19. Waambie pia wachukue kutoka hapa magari ya kukokotwa ya kuwaleta watoto wao wachanga na wake zao na wala wasikose kumleta baba yao.

20. Waambie wasijali juu ya mali zao maana sehemu nzuri kuliko zote katika nchi ya Misri itakuwa yao.”

21. Basi, wana wa Israeli wakafanya kama walivyoagizwa. Yosefu akawapa magari kulingana na maagizo ya Farao na chakula cha njiani.

22. Aliwapa kila mmoja wao mavazi ya kubadili, lakini akampa Benyamini vipande 300 vya fedha na mavazi matano ya kubadili.

23. Tena alimpelekea baba yake zawadi hizi kwa ajili ya safari yake: Punda kumi waliobeba bidhaa bora za Misri, punda jike kumi waliobeba nafaka, mikate na vyakula vingine.

24. Basi, Yosefu akaagana na ndugu zake. Walipokuwa wanaondoka aliwaonya akisema, “Msigombane njiani!”

25. Basi, wakatoka Misri na kurudi nyumbani kwa baba yao Yakobo, nchini Kanaani.

26. Wakamwambia baba yao, “Yosefu yu hai! Yeye ndiye mtawala wa nchi yote ya Misri!” Hapo baba yao akapigwa na bumbuazi, kwani hakuweza kuyasadiki maneno yao.

27. Lakini, walipomsimulia yote waliyoagizwa na Yosefu na alipoyaona magari aliyopelekewa na Yosefu kumchukua, moyo wake ukajaa furaha kupita kiasi.

28. Israeli akasema, “Sasa nimeridhika; mwanangu Yosefu yu hai! Nitakwenda nimwone kabla sijafa.”

Kusoma sura kamili Mwanzo 45