Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 45:11-24 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Utakapokuwa Gosheni, mimi nitakutunza wewe, jamaa yako pamoja na mifugo yako ili msije mkafa njaa, kwani bado miaka mitano zaidi ya njaa.’”

12. Kisha Yosefu akasema, “Nyinyi wenyewe mmeona kwa macho yenu na hata ndugu yangu Benyamini ameona kwa macho yake kwamba ni mimi mwenyewe Yosefu ninayezungumza nanyi.

13. Ni lazima kumwambia baba yangu juu ya fahari yangu huku Misri na yote mliyoyaona. Basi, fanyeni haraka, mkamlete baba yangu huku.”

14. Kisha Yosefu akamkumbatia Benyamini, nduguye, akalia; Benyamini naye akalia, huku wamekumbatiana.

15. Akiwa bado analia, Yosefu akawakumbatia ndugu zake na kuwabusu. Hapo ndipo ndugu zake walipoweza kuzungumza naye.

16. Habari hizo zilipofika ikulu ya mfalme, kwamba ndugu za Yosefu wamekuja, zikamfurahisha sana Farao na watumishi wake.

17. Kwa hiyo, Farao akamwambia Yosefu, “Waambie ndugu zako wawapakie punda wao mizigo, warudi nchini Kanaani,

18. wamlete hapa baba yao na jamaa zao wote. Mimi nitawapa sehemu nzuri kabisa ya nchi ya Misri, ambako wataweza kufurahia matunda yote ya nchi hii.

19. Waambie pia wachukue kutoka hapa magari ya kukokotwa ya kuwaleta watoto wao wachanga na wake zao na wala wasikose kumleta baba yao.

20. Waambie wasijali juu ya mali zao maana sehemu nzuri kuliko zote katika nchi ya Misri itakuwa yao.”

21. Basi, wana wa Israeli wakafanya kama walivyoagizwa. Yosefu akawapa magari kulingana na maagizo ya Farao na chakula cha njiani.

22. Aliwapa kila mmoja wao mavazi ya kubadili, lakini akampa Benyamini vipande 300 vya fedha na mavazi matano ya kubadili.

23. Tena alimpelekea baba yake zawadi hizi kwa ajili ya safari yake: Punda kumi waliobeba bidhaa bora za Misri, punda jike kumi waliobeba nafaka, mikate na vyakula vingine.

24. Basi, Yosefu akaagana na ndugu zake. Walipokuwa wanaondoka aliwaonya akisema, “Msigombane njiani!”

Kusoma sura kamili Mwanzo 45