Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 43:26-34 Biblia Habari Njema (BHN)

26. Yosefu, aliporudi nyumbani, wakamletea zile zawadi walizokuwa nazo, wakamwinamia kwa heshima.

27. Yosefu akawauliza habari zao na kusema, “Mlinisimulia habari za mzee, baba yenu. Je, hajambo? Angali hai?”

28. Wakamjibu, “Mtumishi wako, baba yetu, hajambo na angali hai.” Kisha wakainama kwa heshima.

29. Yosefu alipoinua macho yake na kumwona Benyamini, nduguye, mtoto wa mama yake, akasema, “Huyu ndiye ndugu yenu mdogo mliyeniambia habari zake? Mungu na akufadhili, mwanangu!”

30. Ghafla, Yosefu akatoka mahali hapo, kwani machozi yalikuwa yanamlengalenga kwa shauku kubwa juu ya ndugu yake, akaingia chumbani mwake na kuangua kilio.

31. Baada ya kunawa uso wake, alitoka huku akijikaza, akaamuru chakula kiletwe.

32. Yosefu aliandaliwa chakula chake peke yake, na ndugu zake wakaandaliwa peke yao, hali kadhalika na Wamisri waliokula pamoja naye, wakaandaliwa peke yao, kwani ni chukizo kwa Wamisri kula chakula pamoja na Waebrania.

33. Ndugu zake Yosefu waliketi mbele yake kulingana na umri wao, kuanzia wa kwanza hadi wa mwisho, wakawa wanaangaliana kwa mshangao.

34. Chakula kilikuwa kikichukuliwa kutoka mezani pa Yosefu na kupelekwa kwao, lakini Benyamini alipewa mara tano zaidi ya kiasi walichopewa ndugu zake. Basi, wakanywa na kufurahi pamoja naye.

Kusoma sura kamili Mwanzo 43