Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 40:12-23 Biblia Habari Njema (BHN)

12. Yosefu akamwambia huyo mtumishi, “Tafsiri ya ndoto yako ni hii: Yale matawi matatu ni siku tatu.

13. Baada ya siku tatu Farao atakunyanyua kutoka gerezani na kukurudisha tena katika cheo chako. Utaweza tena kumpa Farao kikombe mkononi kama ulivyokuwa unafanya hapo awali.

14. Lakini tafadhali usinisahau wakati mambo yatakapokwendea vema; unifanyie fadhili na kunitaja mbele ya Farao, nipate kutoka humu gerezani.

15. Maana mimi nilitoroshwa kutoka nchi ya Waebrania, na hapa Misri sijafanya chochote kinachostahili nitiwe gerezani.”

16. Yule mwoka mikate mkuu alipoona kwamba tafsiri ile ni nzuri, akamwambia Yosefu, “Hata mimi niliota ndoto! Katika ndoto yangu nilikuwa nimechukua kichwani nyungo tatu za mikate.

17. Katika ungo wa juu, kulikuwa na vyakula mbalimbali vilivyookwa kwa ajili ya Farao. Lakini, ndege walikuwa wakivila kutoka ungo huo kichwani pangu!”

18. Yosefu akamwambia, “Tafsiri ya ndoto yako ni hii: Zile nyungo tatu ni siku tatu.

19. Baada ya siku tatu Farao atakunyanyua kutoka gerezani, atakiinua kichwa chako akutundike mtini, nao ndege wataula mwili wako.”

20. Mnamo siku ya tatu, ambayo ilikuwa siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwake, Farao aliwaandalia karamu watumishi wake wote. Akawatoa gerezani mtunza vinywaji wake mkuu na mwoka mikate mkuu, akawaweka mbele ya maofisa wake.

21. Kisha akamrudishia cheo chake mtunza vinywaji, apate kumpatia Farao kikombe.

22. Lakini yule mwoka mkate mkuu akamtundika mtini, kama Yosefu alivyokuwa amewatafsiria ndoto zao.

23. Hata hivyo, yule mtunza vinywaji mkuu akamsahau Yosefu, badala ya kumkumbuka.

Kusoma sura kamili Mwanzo 40