Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 40:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Wakati fulani baada ya mambo hayo, maofisa wawili wa mfalme wa Misri walimkosea mfalme. Maofisa hao walikuwa mtunza vinywaji mkuu na mwoka mikate mkuu wa mfalme.

2. Farao aliwakasirikia hao maofisa wake wawili,

3. akawafungia ndani ya ngome ya mkuu wa kikosi cha ulinzi, katika gereza, mahali alipofungwa Yosefu.

4. Mkuu wa kikosi cha ulinzi akamteua Yosefu awatumikie. Nao wakawa kifungoni kwa muda fulani.

5. Basi, usiku mmoja, yule mtunza vinywaji mkuu na yule mwoka mikate mkuu wa mfalme wa Misri, waliota ndoto humo gerezani, kila mmoja na ndoto yake tofauti.

6. Yosefu alipokwenda kwao asubuhi na kuwaona, wote wawili walikuwa wenye wasiwasi.

7. Basi, Yosefu akawauliza maofisa hao wa Farao waliokuwa kifungoni pamoja naye nyumbani mwa bwana wake, “Mbona leo mna nyuso za huzuni?”

8. Wakamjibu, “Tuna huzuni kwa kuwa tumeota ndoto na hakuna awezaye kututafsiria ndoto zetu.” Yosefu akawaambia, “Je, kutafsiri ndoto si kazi ya Mungu? Basi, niambieni ndoto zenu.”

9. Mtunza vinywaji mkuu wa mfalme akamsimulia Yosefu ndoto yake, akisema, “Katika ndoto yangu niliona mzabibu mbele yangu,

10. nao ulikuwa na matawi matatu. Mara tu ulipoanza kuchipua majani, maua yake yalichanua na vishada vyake vikawa zabibu mbivu.

11. Mkononi mwangu nilikuwa na kikombe cha Farao, basi, nikazitwaa zabibu, nikazikamua katika kikombe hicho, nikampa Farao.”

12. Yosefu akamwambia huyo mtumishi, “Tafsiri ya ndoto yako ni hii: Yale matawi matatu ni siku tatu.

Kusoma sura kamili Mwanzo 40