Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 4:10-24 Biblia Habari Njema (BHN)

10. Mwenyezi-Mungu akasema, “Umefanya nini? Damu ya ndugu yako yanililia kutoka udongoni.

11. Sasa wewe umelaaniwa! Hutailima tena ardhi yenye rutuba ambayo kama kinywa imeipokea damu ya nduguyo uliyemuua.

12. Ukiilima ardhi haitakupatia tena mazao yake. Utakuwa mtu wa kutangatanga, asiye na makao maalumu duniani.”

13. Kaini akamwambia Mwenyezi-Mungu, “Adhabu yangu ni kubwa mno; siwezi kuistahimili.

14. Leo umenifukuza kutoka ardhi yenye rutuba na mbali nawe. Basi, nitakuwa mtu wa kutangatanga, asiye na makao maalumu duniani, na yeyote atakayeniona ataniua.”

15. Lakini Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Sivyo! Atakayekuua wewe Kaini atalipizwa mara saba.” Basi, Mwenyezi-Mungu akamtia Kaini alama ya tahadhari, ili yeyote atakayemwona asimuue.

16. Kisha Kaini akaondoka mbele ya Mwenyezi-Mungu, akawa anaishi katika nchi ya Nodi, upande wa mashariki wa Edeni.

17. Kaini akalala na mkewe, naye akapata mimba, akamzaa Henoki. Kaini akajenga mji akauita kwa jina la Henoki mwanawe.

18. Henoki akamzaa Iradi, naye Iradi akamzaa Mehuyaeli; Mehuyaeli akamzaa Methushaeli, naye Methushaeli akamzaa Lameki.

19. Lameki alioa wanawake wawili, mmoja aliitwa Ada na mwingine Sila.

20. Ada alimzaa Yabali ambaye alikuwa baba yao wafugaji waishio mahemani.

21. Ndugu yake alikuwa Yubali; huyo alikuwa baba yao wanamuziki wote wapigao zeze na filimbi.

22. Sila naye alimzaa Tubal-kaini, ambaye alikuwa mhunzi wa vyombo vyote vya shaba na chuma. Dada yake Tubal-kaini alikuwa Naama.

23. Lameki akawaambia wake zake,“Ada na Sila sikieni sauti yangu!Sikilizeni nisemayo enyi wake za Lameki.Mimi niliua mtu kwa kunijeruhi,naam, nilimuua kijana kwa kuniumiza.

24. Ikiwa Kaini atalipizwa mara saba,kweli Lameki atalipizwa mara sabini na saba.”

Kusoma sura kamili Mwanzo 4