Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 39:8-23 Biblia Habari Njema (BHN)

8. Lakini Yosefu akakataa na kumwambia huyo bwana wake, “Kamwe! Bwana wangu amenipa mamlaka juu ya kila kitu hapa nyumbani na, kwa vile niko, hajishughulishi na kitu chochote tena.

9. Hapa nyumbani yeye hana madaraka kuliko mimi. Yeye hakunikataza kushika chochote isipokuwa wewe tu kwa kuwa wewe ni mke wake. Nitawezaje basi kufanya uovu mbaya kama huo, na kumkosea Mungu.”

10. Huyo mwanamke aliendelea kumshawishi Yosefu siku baada ya siku, lakini Yosefu hakumsikiliza wala kukubali kulala naye kamwe.

11. Siku moja, Yosefu aliingia nyumbani kufanya kazi yake kama kawaida, na wafanyakazi wengine hawakuwamo nyumbani.

12. Basi, mke wa Potifa alimshika joho lake na kumwambia, “Lala na mimi!” Lakini Yosefu akamwachia vazi lake mikononi mwake, akakimbilia nje.

13. Hapo, yule mwanamke alipoona kwamba Yosefu ameliacha vazi lake mikononi mwake na kukimbilia nje,

14. akawaita watumishi wa nyumbani mwake na kuwaambia, “Tazameni! Huyu Mwebrania tuliyeletewa anatuaibisha. Alikuja kwangu akitaka kunishika kwa nguvu, lakini nikapiga kelele.

15. Aliposikia napiga kelele, aliliacha vazi lake, akakimbilia nje!”

16. Basi, yule mwanamke akaliweka vazi hilo mpaka mumewe aliporudi nyumbani.

17. Akamsimulia kisa kile akisema, “Huyu mtumishi Mwebrania uliyemleta kwetu alinijia ili kuniaibisha.

18. Lakini mara tu nilipopiga kelele, aliliacha vazi lake na kukimbilia nje.”

19. Basi, bwana wake Yosefu alipoyasikia maneno ya mkewe, kwamba ndivyo mtumishi wake alivyomtendea, akawaka hasira,

20. akamchukua Yosefu na kumtia gerezani, mahali walipofungwa wahalifu wa mfalme.

21. Lakini hata humo gerezani Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na Yosefu akimfadhili hata kumfanya apendeke mbele ya mkuu wa gereza.

22. Hivyo mkuu wa gereza alimweka Yosefu awe mkuu wa wafungwa wote humo gerezani; kila kitu kilichofanyika humo kilifanywa kwa mamlaka yake.

23. Huyo mkuu wa gereza hakujishughulisha tena na kitu chochote alichokabidhiwa Yosefu kwa maana Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na Yosefu na kufanikisha kila kitu alichofanya.

Kusoma sura kamili Mwanzo 39