Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 38:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Wakati huo, Yuda alitengana na ndugu zake, akaenda kukaa na mtu mmoja Mwadulami, jina lake Hira.

2. Akiwa huko, Yuda akamwona binti Shua, Mkanaani, akamwoa.

3. Binti Shua akapata mimba akazaa mtoto wa kiume, Yuda akamwita Eri.

4. Akapata mimba nyingine, akajifungua mtoto wa kiume, akamwita Onani.

5. Kisha akapata mtoto mwingine wa kiume, akamwita Shela. Wakati Shela alipozaliwa, Yuda alikuwa Kezibu.

6. Baadaye Yuda alimwoza mtoto wake wa kwanza Eri, kwa mwanamke aitwaye Tamari.

7. Lakini Eri, mzaliwa wa kwanza wa Yuda, alikuwa mwovu mbele ya Mwenyezi-Mungu; hivyo Mwenyezi-Mungu akamuua.

8. Basi, Yuda akamwambia Onani, “Mchukue mke wa ndugu yako marehemu, kwani ndivyo inavyokupasa kufanya, upate kumzalia nduguyo watoto.”

9. Lakini Onani alijua kwamba hao watoto wasingekuwa wake. Kwa hiyo, alipolala na mke wa nduguye, alimwaga chini mbegu ya uzazi, asije akampatia nduguye watoto.

10. Tendo hilo likamwudhi Mwenyezi-Mungu, akamuua Onani pia.

11. Ndipo Yuda akamwambia Tamari, mke wa mwanawe, “Rudi nyumbani kwa baba yako, ubaki mjane hadi mwanangu Shela atakapokua.” Yuda alihofu Shela naye asije akafa kama ndugu zake. Basi, Tamari akarudi nyumbani kwa baba yake.

12. Kisha binti Shua, mkewe Yuda, akafariki. Yuda alipomaliza kufanya matanga akaondoka na rafiki yake Hira, Mwadulami, wakaenda Timna kwa wakata-manyoya ya kondoo wake.

Kusoma sura kamili Mwanzo 38