Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 37:9-20 Biblia Habari Njema (BHN)

9. Kisha Yosefu akaota ndoto nyingine, akawasimulia ndugu zake akisema, “Sikilizeni, nimeota ndoto nyingine; nimeona jua, mwezi na nyota kumi na moja vinaniinamia.”

10. Lakini alipomsimulia baba yake na ndugu zake ndoto hiyo, baba yake alimkemea akisema, “Ni ndoto gani hiyo uliyoota? Je, itatulazimu mimi, mama yako na ndugu zako kuja kuinama chini kwa heshima mbele yako?”

11. Ndugu zake wakamwonea wivu, lakini baba yake akawa analifikiria jambo hilo.

12. Siku moja, ndugu zake Yosefu walikwenda kuchunga wanyama wa baba yao karibu na Shekemu.

13. Basi, Israeli akamwambia Yosefu, “Unajua ndugu zako wanachunga wanyama kule Shekemu. Kwa hiyo nataka nikutume kwao.” Yosefu akajibu, “Niko tayari.”

14. Baba yake akamwambia, “Nenda ukawaangalie ndugu zako na wanyama kama wako salama, kisha uniletee habari.” Basi, Yakobo akamtuma Yosefu kutoka bonde la Hebroni. Yosefu alipokaribia Shekemu

15. mtu mmoja akamkuta akitangatanga mbugani, akamwuliza, “Unatafuta nini?”

16. Yosefu akamjibu, “Ninawatafuta ndugu zangu. Tafadhali, niambie mahali wanakochunga wanyama.”

17. Yule mtu akamwambia, “Bila shaka wamekwisha ondoka, kwa sababu niliwasikia wakisema kwamba wanakwenda Dothani.” Basi, Yosefu akawafuata ndugu zake, akawakuta huko Dothani.

18. Ndugu zake walipomwona akiwa mbali na kabla hajafika karibu, wakafanya mpango wa kumuua.

19. Waliambiana, “Tazameni! Yule mwota ndoto anakuja.

20. Haya, tumuue na kumtupa ndani ya shimo mojawapo. Baadaye tutasema kwamba ameuawa na mnyama wa porini. Halafu tutaona hizo ndoto zake zitakuwaje.”

Kusoma sura kamili Mwanzo 37