Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 31:39-53 Biblia Habari Njema (BHN)

39. Mimi sikukuletea hata mara moja mnyama wako aliyeuawa na mnyama wa porini, bali nilifidia hasara hiyo mimi mwenyewe. Wewe ulinitaka nilipe bila kujali kama aliibiwa mchana au usiku!

40. Hivyo, mchana nilistahimili jua kali na usiku baridi ilinipiga hata nisiweze kupata usingizi hata kidogo.

41. Kwa miaka ishirini hii yote nimeishi nyumbani kwako. Nilikutumikia miaka kumi na minne kwa ajili ya binti zako wawili, na miaka sita nikawachunga wanyama wako. Lakini wewe, ukabadilisha ujira wangu mara kumi.

42. Kama Mungu wa babu yangu Abrahamu, Mungu ambaye alimfanya baba yangu Isaka kutetemeka, asingelikuwa upande wangu, hakika ungeliniacha niondoke mikono mitupu. Lakini Mungu aliyaona mateso yangu na kazi niliyofanya kwa mikono yangu, akakukemea usiku wa kuamkia leo.”

43. Hapo Labani akamjibu Yakobo, “Binti hawa ni binti zangu, watoto hawa ni watoto wangu, wanyama hawa ni wanyama wangu, na yote unayoyaona hapa ni yangu. Lakini mimi ninaweza kufanya nini leo juu ya hawa binti zangu na watoto wao waliowazaa?

44. Basi, tufanye agano mimi nawe, liwe ushahidi kati yako nami.”

45. Basi, Yakobo akachukua jiwe, akalisimika kama nguzo ya ukumbusho.

46. Tena Yakobo akawaambia ndugu zake, “Kusanyeni mawe.” Nao wakakusanya mawe na kufanya rundo. Kisha wakala chakula karibu na rundo hilo la mawe.

47. Labani akaliita rundo hilo Yegar-sahadutha, lakini Yakobo akaliita Galeedi.

48. Labani akasema, “Rundo hili ni ushahidi kati yako na mimi leo.” Kwa hiyo Labani akaliita Galeedi,

49. na ile nguzo akaiita Mizpa akisema, “Mwenyezi-Mungu na atulinde tuwapo mbali bila kuonana.

50. Kama ukiwatesa binti zangu, au ukioa wanawake wengine zaidi ya hawa, basi ujue kwamba hakuna aliye shahidi kati yetu ila Mungu mwenyewe.”

51. Halafu Labani akamwambia Yakobo, “Tazama rundo hili la mawe na nguzo ambayo nimeisimika kati yako nami.

52. Rundo hili ni ushahidi na nguzo hii ni ushahidi kwamba mimi sitavuka rundo hili kuja kwako kukudhuru, na wala wewe hutavuka rundo hili na nguzo hii kuja kwangu kunidhuru.

53. Mungu wa Abrahamu na Mungu wa Nahori, ataamua kati yetu.” Basi, Yakobo akaapa kwa Mungu ambaye alimfanya baba yake Isaka, kutetemeka.

Kusoma sura kamili Mwanzo 31