Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 3:5-15 Biblia Habari Njema (BHN)

5. Mungu alisema hivyo kwa sababu anajua kwamba mkila matunda ya mti huo mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.”

6. Basi, mwanamke alipoona kuwa mti huo ni mzuri kwa chakula, wavutia macho, na kwamba wafaa kwa kupata hekima, akachuma tunda lake, akala, akampa na mumewe, naye pia akala.

7. Mara macho yao yakafumbuliwa, wakatambua kwamba wako uchi; hivyo wakajishonea majani ya mtini, wakajifanyia mavazi ya kiunoni.

8. Jioni, wakati wa kupunga upepo, huyo mwanamume na mkewe wakasikia hatua za Mwenyezi-Mungu akitembea bustanini, nao wakajificha kati ya miti ya bustani, Mwenyezi-Mungu asipate kuwaona.

9. Lakini Mwenyezi-Mungu akamwita huyo mwanamume, “Uko wapi?”

10. Naye akamjibu, “Nimesikia hatua zako bustanini, nikaogopa na kujificha, maana nilikuwa uchi.”

11. Mwenyezi-Mungu akamwuliza, “Nani aliyekuambia kwamba uko uchi? Je, umekula tunda la mti nililokuamuru usile?”

12. Huyo mwanamume akajibu, “Mwanamke uliyenipa akae pamoja nami ndiye aliyenipa tunda la mti huo, nami nikala.”

13. Hapo Mwenyezi-Mungu akamwuliza huyo mwanamke, “Umefanya nini wewe?” Mwanamke akamjibu, “Nyoka alinidanganya, nami nikala.”

14. Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia nyoka,“Kwa kuwa umefanya hivyo,umelaaniwa kuliko wanyama wote wa kufugwa,na kuliko wanyama wote wa porini.Kwa tumbo lako utatambaa,na kula vumbi siku zote za maisha yako.

15. Nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke,kati ya uzawa wako na uzawa wake;yeye atakiponda kichwa chako,nawe utamwuma kisigino chake.”

Kusoma sura kamili Mwanzo 3