Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 27:20-33 Biblia Habari Njema (BHN)

20. Lakini Isaka akamwuliza, “Imekuwaje umepata mawindo upesi hivyo, mwanangu?” Yakobo akamjibu, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, amenifanikisha.”

21. Ndipo Isaka akamwambia Yakobo, “Basi, mwanangu, karibia nipate kukupapasa ili nijue kweli kama wewe ndiwe mwanangu Esau au la.”

22. Yakobo akamkaribia baba yake Isaka, naye akampapasa na kusema, “Sauti ni sauti ya Yakobo, lakini mikono ni mikono ya Esau.”

23. Hakumtambua kwa sababu mikono yake ilikuwa yenye nywele nyingi kama ya Esau kaka yake; kwa hiyo akambariki.

24. Akamwuliza tena, “Kweli wewe ndiwe mwanangu Esau?” Naye akamjibu, “Ndiyo.”

25. Basi, baba yake akasema, “Niletee hiyo nyama nile mawindo yako mwanangu, nikubariki.” Hapo Yakobo akampelekea chakula, naye akala; akampelekea divai pia, akanywa.

26. Ndipo baba yake Isaka, akamwambia, “Sogea karibu, mwanangu, unibusu.”

27. Basi, Yakobo akamkaribia baba yake na kumbusu, na baba yake aliposikia harufu ya mavazi yake, akambariki akisema,“Tazama, harufu nzuri ya mwananguni kama harufu ya shamba alilobariki Mwenyezi-Mungu!

28. Mungu akumiminie umande wa mbinguni;akupe ardhi yenye rutuba,nafaka na divai kwa wingi.

29. Jamii za watu zikutumikie,na mataifa yakuinamie kwa heshima.Uwe mtawala wa ndugu zako,watoto wa kiume wa mama yako wakuinamie kwa heshima.Kila akulaaniye na alaaniwe,kila akubarikiye na abarikiwe!”

30. Isaka alipokwisha kumbariki Yakobo, naye Yakobo alipokuwa ndio tu ametoka mbele ya baba yake Isaka, Esau kaka yake Yakobo, akarudi kutoka mawindoni.

31. Esau pia akatengeneza chakula kitamu, akampelekea baba yake, akamwambia, “Haya baba, inuka ule mawindo yangu mimi mwanao, ili upate kunibariki!”

32. Isaka akauliza, “Wewe ni nani?” Naye akamjibu, “Ni mimi mwanao Esau, mzaliwa wako wa kwanza.”

33. Hapo Isaka akatetemeka mno, akasema, “Ni nani basi yule aliyewinda na kuniletea mawindo, nami nimekwisha kula kabla hujaja? Tena nimekwisha mbariki; naam, amekwisha barikiwa!”

Kusoma sura kamili Mwanzo 27