Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 27:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Isaka alikuwa amezeeka na macho yake yalikuwa hayaoni. Basi, alimwita Esau mwanawe mkubwa, akamwambia, “Mwanangu!” Naye akaitika “Naam baba, nasikiliza!”

2. Isaka akasema, “Tazama, mimi ni mzee, wala siku ya kufa kwangu siijui.

3. Basi, chukua silaha zako, yaani podo na upinde wako, uende porini ukaniwindie mnyama.

4. Halafu unitengenezee chakula kitamu, kile nipendacho, uniletee ili nile, nipate kukubariki kabla ya kufa kwangu.”

5. Kumbe, wakati huo Isaka alipokuwa akiongea na Esau mwanawe, Rebeka alikuwa anasikiliza. Kwa hiyo, Esau alipokwenda porini kuwinda,

6. Rebeka alimwambia mwanawe Yakobo, “Nimemsikia baba yako akimwambia kaka yako Esau,

7. amwindie mnyama na kumtengenezea chakula kitamu, ili ale, apate kumbariki mbele ya Mwenyezi-Mungu kabla ya kufa kwake.

8. Sasa mwanangu, sikiliza maneno yangu na utii ninayokuagiza.

9. Nenda kwenye kundi la mbuzi uniletee wanambuzi wawili wazuri, nimtengenezee baba yako chakula kitamu, kile apendacho.

10. Kisha utampelekea baba yako ale, apate kukubariki kabla hajafa.”

11. Lakini Yakobo akamwambia mama yake Rebeka, “Kumbuka kaka yangu Esau amejaa nywele mwilini, hali mimi sina.

12. Labda baba atataka kunipapasa, nami nitaonekana kama ninamdhihaki, kwa hiyo nitajiletea laana badala ya baraka.”

Kusoma sura kamili Mwanzo 27