Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 26:12-21 Biblia Habari Njema (BHN)

12. Mwaka huo Isaka alipanda mbegu katika nchi ile, akavuna mara mia zaidi, maana Mwenyezi-Mungu alimbariki,

13. naye akatajirika. Alizidi kupata mali hadi akawa tajiri sana.

14. Alikuwa na makundi ya kondoo, ng'ombe na watumwa wengi, hata Wafilisti wakamwonea wivu.

15. Wafilisti walikuwa wamevifukia visima vyote vya maji ambavyo watumishi wa Abrahamu, baba yake, walikuwa wamechimba wakati alipokuwa bado hai.

16. Ndipo Abimeleki akamwambia Isaka, “Ondoka kwetu, kwani wewe umetuzidi nguvu.”

17. Basi, Isaka akaondoka huko, akapiga kambi yake katika bonde la Gerari, akakaa huko.

18. Isaka akavichimbua vile visima vilivyokuwa vimechimbwa wakati Abrahamu baba yake alipokuwa hai, visima ambavyo Wafilisti walikuwa wamevifukia baada ya kifo cha Abrahamu. Akavipa majina yaleyale aliyovipa baba yake.

19. Lakini watumishi wa Isaka walipochimba katika lile bonde na kupata kisima cha maji yanayobubujika,

20. wachungaji wa hapo Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, “Maji haya ni yetu.” Hivyo Isaka akakiita kisima hicho Eseki, kwa sababu waligombana naye.

21. Halafu wakachimba kisima kingine, nacho pia wakakigombania; hivyo Isaka akakiita kisima hicho Sitna.

Kusoma sura kamili Mwanzo 26