Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 24:14-25 Biblia Habari Njema (BHN)

14. Basi, msichana nitakayemwambia atue mtungi wake wa maji anipatie maji ninywe, naye akanipa mimi pamoja na kuwanywesha ngamia wangu, na awe ndiye uliyemchagulia mtumishi wako Isaka. Jambo hilo litanionesha kwamba umemfadhili bwana wangu.”

15. Kabla hajamaliza kuomba, mara Rebeka, binti Bethueli, mwana wa Milka, mkewe Nahori, ndugu yake Abrahamu, akafika amebeba mtungi wake begani.

16. Msichana huyo alikuwa na sura ya kuvutia sana, na bikira ambaye hakuwa amelala na mwanamume yeyote. Basi, akateremka kisimani, akaujaza mtungi wake maji na kupanda.

17. Ndipo yule mtumishi akaharakisha kukutana naye, akamwambia, “Tafadhali, nipatie maji ya kunywa kutoka mtungi wako.”

18. Msichana akamjibu, “Haya kunywa bwana wangu.” Na papo hapo akautua mtungi wake, akiushikilia ili amnyweshe.

19. Alipokwisha kumpatia maji, akamwambia, “Nitawatekea maji ngamia wako pia, wanywe mpaka watosheke.”

20. Basi, akafanya haraka, akawamiminia ngamia maji ya mtungi wake katika hori, akakimbia kisimani kuteka maji mengine na kuwanywesha ngamia wake wote.

21. Yule mtu akawa anamtazama kwa makini bila kusema lolote, apate kufahamu kama Mwenyezi-Mungu ameifanikisha safari yake au sivyo.

22. Ngamia walipotosheka kunywa maji, yule mtu akampa huyo msichana pete ya dhahabu yenye uzito upatao gramu sita, na bangili mbili za dhahabu za gramu kumi kila moja.

23. Akamwuliza, “Niambie tafadhali: Wewe ni binti nani? Je, kuna nafasi ya kulala nyumbani kwenu?”

24. Rebeka akajibu, “Mimi ni binti Bethueli, mwana wa Milka, mkewe Nahori.

25. Kwetu kuna majani na malisho ya kutosha na mahali pa kulala wageni.”

Kusoma sura kamili Mwanzo 24