Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 22:11-24 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Lakini malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwita kutoka mbinguni, “Abrahamu! Abrahamu!” Naye akaitika, “Naam, nasikiliza!”

12. Malaika akamwambia, “Usimdhuru mtoto wala usimfanye lolote! Sasa ninajua kwamba unamcha Mungu, kwani hukuninyima hata mwanao wa pekee.”

13. Ndipo Abrahamu akatazama, akaona kondoo dume amenaswa pembe zake kichakani. Basi, akaenda, akamchukua huyo kondoo, akamtoa sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe.

14. Kwa hiyo, Abrahamu akapaita mahali hapo, “Mwenyezi-Mungu hujalia.” Kama isemwavyo hata leo, “Katika mlima wa Mwenyezi-Mungu, watu hujaliwa.”

15. Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwita Abrahamu mara ya pili kutoka mbinguni,

16. akamwambia, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: Nimeapa kwa nafsi yangu kwamba kwa kuwa umefanya hivi, wala hukuninyima mwanao wa pekee,

17. hakika nitakubariki, na wazawa wako nitawazidisha kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ufuoni mwa bahari. Wazawa wako wataimiliki miji ya adui zao.

18. Kutokana na wazawa wako mataifa yote duniani yatabarikiwa kwa sababu wewe umeitii amri yangu.”

19. Basi, Abrahamu akawarudia wale watumishi wake, nao kwa pamoja wakaondoka, wakarudi Beer-sheba; Abrahamu akakaa huko Beer-sheba.

20. Baada ya matukio hayo Abrahamu alipata habari kwamba Milka pia amemzalia Nahori, nduguye, watoto wa kiume:

21. Usi mzaliwa wa kwanza, Buzi ndugu yake, Kemueli baba yake Aramu,

22. Kesedi, Hazo, Pildashi, Yidlafu na Bethueli.

23. Bethueli alimzaa Rebeka. Milka alimzalia Nahori, ndugu yake Abrahamu, watoto hao wanane.

24. Zaidi ya hayo, Reuma, suria wa Nahori, pia alimzalia watoto: Teba, Gahamu, Tahashi na Maaka.

Kusoma sura kamili Mwanzo 22