Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 21:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mwenyezi-Mungu alimkumbuka Sara, akamtendea kama alivyoahidi.

2. Basi, Abrahamu akiwa mzee, Sara akapata mimba, akamzalia mtoto wa kiume, wakati uleule Mungu alioutaja.

3. Abrahamu akampa huyo mwanawe ambaye Sara alimzalia jina Isaka.

4. Isaka alipotimiza umri wa siku nane, Abrahamu akamtahiri kama alivyoamriwa na Mungu.

5. Abrahamu alikuwa na umri wa miaka 100 wakati mwanawe Isaka alipozaliwa.

6. Naye Sara akasema, “Mungu amenipatia kicheko; yeyote atakayesikia habari hizi, atacheka pamoja nami.”

7. Kisha akaongeza, “Ni nani angeweza kumwambia Abrahamu kwamba mimi Sara nitanyonyesha watoto? Tena nimemzalia mtoto wa kiume katika uzee wake!”

8. Isaka akaendelea kukua, na siku alipoachishwa kunyonya, Abrahamu akafanya sherehe kubwa.

9. Baadaye Sara alimwona Ishmaeli, mtoto wa Abrahamu aliyezaliwa na Hagari, Mmisri, akicheza na Isaka mwanawe.

10. Basi, Sara akamwambia Abrahamu, “Mfukuzie mbali mjakazi huyu na mwanawe. Haiwezekani kabisa mtoto wa mjakazi kurithi pamoja na mwanangu Isaka.”

11. Jambo hili lilimhuzunisha sana Abrahamu kwa kuwa Ishmaeli pia alikuwa mtoto wake.

12. Lakini Mungu akamwambia Abrahamu, “Usihuzunike kwa sababu ya mtoto huyu, wala huyo mtumwa wako wa kike. Lolote akuambialo Sara lifanye; kwa kweli wazawa wako watatokana na Isaka.

Kusoma sura kamili Mwanzo 21