Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 2:2-14 Biblia Habari Njema (BHN)

2. Siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyofanya; siku hiyo ya saba Mungu akapumzika baada ya kazi yake yote aliyofanya.

3. Mungu akaibariki siku ya saba na kuitakasa, kwa kuwa siku hiyo Mungu alipumzika baada ya kazi yake yote ya kuumba.

4. Hivyo ndivyo mbingu na dunia zilivyoumbwa.Siku ile Mwenyezi-Mungu alipoziumba mbingu na dunia,

5. Hapakuwa na mimea juu ya nchi wala miti haikuwa imechipua kwani Mwenyezi-Mungu hakuwa ameinyeshea nchi mvua, wala hapakuwa na mtu wa kuilima.

6. Hata hivyo, maji yalitoka ardhini yakainywesha ardhi yote.

7. Basi, Mwenyezi-Mungu akamfanya mwanamume kwa mavumbi ya udongo, akampulizia puani pumzi ya uhai, na huyo mwanamume akawa kiumbe hai.

8. Kisha Mwenyezi-Mungu akapanda bustani huko Edeni, upande wa mashariki, na humo akamweka huyo mwanamume aliyemuumba.

9. Mwenyezi-Mungu akaotesha kutoka ardhini kila aina ya miti mizuri izaayo matunda yafaayo kwa chakula. Katikati ya bustani hiyo kulikuwa na mti wa uhai na mti wa ujuzi wa mema na mabaya.

10. Kulikuwa na mto huko Edeni uliotiririka maji na kuinywesha hiyo bustani; kutoka huko mto huo uligawanyika kuwa mito minne.

11. Jina la mto wa kwanza ni Pishoni; huo waizunguka nchi yote ya Hawila ambako kuna dhahabu.

12. Dhahabu ya nchi hiyo ni safi kabisa. Huko pia kuna marashi yaitwayo bedola na vito viitwavyo shohamu.

13. Jina la mto wa pili ni Gihoni; huo waizunguka nchi yote ya Kushi.

14. Jina la mto wa tatu ni Tigri, nao watiririkia upande wa mashariki wa nchi ya Ashuru; na jina la mto wa nne ni Eufrate.

Kusoma sura kamili Mwanzo 2