Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 16:5-14 Biblia Habari Njema (BHN)

5. Sarai akamwambia Abramu, “Wewe utawajibika kwa ubaya ninaotendewa. Mimi nilikupa mjakazi wangu, lakini alipopata mimba, mimi nimekuwa duni machoni pake! Mwenyezi-Mungu na ahukumu kati yako na mimi!”

6. Lakini Abramu akamwambia Sarai, “Mjakazi wako yuko chini ya mamlaka yako; mfanyie upendavyo.” Basi, Sarai akamtesa Hagari mpaka akatoroka.

7. Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamkuta Hagari penye chemchemi ya maji jangwani, chemchemi iliyoko njiani kuelekea Shuri.

8. Malaika akamwuliza, “Hagari, mjakazi wa Sarai! Unatoka wapi na unakwenda wapi?” Hagari akamjibu, “Namkimbia bimkubwa wangu Sarai.”

9. Yule malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Rudi kwa bimkubwa wako Sarai na umtii.”

10. Zaidi ya hayo, malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia Hagari, “Nitawazidisha wazawa wako hata wasiweze kuhesabika kwa wingi wao.”

11. Kisha huyo malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Wewe ni mjamzito na utajifungua mtoto wa kiume; utamwita Ishmaeli, maana Mwenyezi-Mungu amesikia mateso yako.

12. Ishmaeli ataishi kama pundamwitu; atakuwa adui wa kila mtu na kila mtu atakuwa adui yake. Ataishi akiwa adui wa jamaa yake.”

13. Basi, Hagari akampa jina Mwenyezi-Mungu aliyezungumza naye huko, “Wewe ni Mungu Aonaye” kwa maana alifikiri, “Kweli hapa nimemwona yeye anionaye!”

14. Ndiyo maana kile kisima chaitwa Beer-lahai-roi. Kisima hiki kipo kati ya Kadeshi na Beredi.

Kusoma sura kamili Mwanzo 16