Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 15:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Baada ya mambo hayo, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Abramu katika maono, “Abramu! Usiogope! Mimi ni ngao yako. Tuzo lako litakuwa kubwa!”

2. Lakini Abramu akasema, “Ee Mwenyezi-Mungu, utanipa nini hali naendelea kuishi bila mtoto, na mrithi wangu ni Eliezeri wa Damasko?

3. Tazama! Hujanijalia mtoto; mtumwa aliyezaliwa nyumbani mwangu ndiye atakayekuwa mrithi wangu!”

4. Ndipo Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Huyu hatakuwa mrithi wako! Mwanao halisi ndiye atakayekuwa mrithi wako.”

5. Hapo Mwenyezi-Mungu akamleta Abramu nje na kumwambia, “Tazama mbinguni! Zihesabu nyota, kama kweli utaweza kuzihesabu! Hivyo ndivyo wazawa wako watakavyokuwa wengi!”

6. Abramu akamwamini Mwenyezi-Mungu, naye Mwenyezi-Mungu akamkubali Abramu kuwa mwadilifu.

7. Mwenyezi-Mungu akamwambia Abramu, “Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu niliyekuleta toka Uri, mji wa Wakaldayo, ili nikupe nchi hii uimiliki.”

8. Lakini Abramu akamwambia, “Ee Mwenyezi-Mungu, nitajuaje kwamba nitaimiliki nchi hii?”

9. Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Niletee ndama wa miaka mitatu, mwanambuzi jike wa miaka mitatu, kondoo dume wa miaka mitatu, na hua na kinda la njiwa.”

10. Abramu akamletea hao wote, akamkata kila mnyama vipande viwili, akavipanga katika safu mbili, vikielekeana; lakini ndege hakuwakata vipande viwili.

11. Na tai walipoijia hiyo mizoga, Abramu akawa anawafukuza.

Kusoma sura kamili Mwanzo 15