Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 14:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Wakati huo, mfalme Amrafeli wa Shinari, mfalme Arioko wa Elasari, mfalme Kedorlaomeri wa Elamu na mfalme Tidali wa Goiimu,

2. walipigana vita dhidi ya Bera mfalme wa Sodoma, dhidi ya Birsha mfalme wa Gomora, Shinabu mfalme wa Adma, Shemeberi mfalme wa Seboimu, na dhidi ya mfalme wa Bela (yaani Soari).

3. Wafalme hao watano waliyaunganisha majeshi yao katika bonde la Sidimu (yaani Bahari ya Chumvi).

4. Kwa muda wa miaka kumi na miwili walikuwa wakimtii mfalme Kedorlaomeri, lakini mnamo mwaka wa kumi na tatu, walimwasi.

5. Mnamo mwaka wa kumi na nne, mfalme Kedorlaomeri na wale wafalme wenzake walikuja na kuwashinda watu wa Refaimu huko Ashtaroth-karnaimu, na Wazuzi huko Hamu, na Waemi huko Shawe-kiriathaimu,

6. na Wahori huko mlimani kwao Seiri, wakawafukuza hadi Elparani, mpakani mwa jangwa.

7. Kisha wakarudi nyuma mpaka Enmishpati (yaani Kadeshi), wakaivamia nchi yote ya Waamaleki, na kuwashinda Waamori waliokaa Hasason-tamari.

8. Ndipo mfalme wa Sodoma, mfalme wa Gomora, mfalme wa Adma, mfalme wa Seboimu na mfalme wa Bela

9. (yaani Soari), wakaingia vitani katika bonde la Sidimu kupigana na Kedorlaomeri mfalme wa Elamu, Tidali mfalme wa Goiimu, Amrafeli mfalme wa Shinari na Arioko mfalme wa Elasari; wafalme wanne dhidi ya wafalme watano.

10. Bonde la Sidimu lilikuwa limejaa mashimo ya lami; kwa hiyo wafalme wa Sodoma na Gomora walipokuwa wakiikimbia vita, wakatumbukia humo, lakini wengine wakatorokea mlimani.

11. Basi, wale walioshinda, wakateka mali yote ya Sodoma na Gomora, kadhalika na mazao yao, wakaenda zao.

12. Walimteka hata Loti, mwana wa nduguye Abramu aliyekuwa anakaa Sodoma, pamoja na mali yake, wakaenda zao.

13. Mtu mmoja aliyeponyoka, akaenda kumwarifu yule Mwebrania Abramu ambaye alikuwa anaishi karibu na mialoni ya Mwamori Mamre. Mamre alikuwa ndugu yake Eshkoli na Aneri. Wote walikuwa wamefanya agano na Abramu.

Kusoma sura kamili Mwanzo 14