Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 1:16-26 Biblia Habari Njema (BHN)

16. Basi, Mungu akafanya mianga miwili mikubwa; ule mkubwa utawale mchana na ule mdogo utawale usiku; akafanya na nyota pia.

17. Mungu akaiweka mianga hiyo angani iiangazie dunia,

18. ipate kutawala mchana na usiku, na kuutenga mwanga na giza. Mungu akaona kuwa ni vyema.

19. Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya nne.

20. Mungu akasema, “Maji na yatoe makundi ya viumbe hai na ndege waruke angani.”

21. Basi, Mungu akaumba wanyama wakubwa sana wa baharini na aina zote za viumbe vyote hai viendavyo na kujaa majini; akaumba na aina zote za ndege wote. Mungu akaona kuwa ni vyema.

22. Mungu akavibariki, akasema, “Zaeni, muongezeke, muyajaze maji ya bahari; nao ndege waongezeke katika nchi.”

23. Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya tano.

24. Mungu akasema, “Nchi na itoe aina zote za viumbe hai, wanyama wa kufugwa, viumbe vitambaavyo na wanyama wa porini wa kila aina.” Ikawa hivyo.

25. Basi, Mungu akafanya aina zote za wanyama wa porini, wanyama wa kufugwa, na viumbe vitambaavyo. Mungu akaona kuwa ni vyema.

26. Kisha Mungu akasema, “Tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; atawale samaki wa baharini, ndege wa angani, wanyama wa kufugwa, dunia yote na viumbe vyote vitambaavyo.”

Kusoma sura kamili Mwanzo 1