Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 1:13-31 Biblia Habari Njema (BHN)

13. Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya tatu.

14. Mungu akasema, “Mianga na iweko angani, itenge mchana na usiku, ioneshe nyakati, majira, siku na miaka,

15. na ingae angani na kuiangazia dunia.” Ikawa hivyo.

16. Basi, Mungu akafanya mianga miwili mikubwa; ule mkubwa utawale mchana na ule mdogo utawale usiku; akafanya na nyota pia.

17. Mungu akaiweka mianga hiyo angani iiangazie dunia,

18. ipate kutawala mchana na usiku, na kuutenga mwanga na giza. Mungu akaona kuwa ni vyema.

19. Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya nne.

20. Mungu akasema, “Maji na yatoe makundi ya viumbe hai na ndege waruke angani.”

21. Basi, Mungu akaumba wanyama wakubwa sana wa baharini na aina zote za viumbe vyote hai viendavyo na kujaa majini; akaumba na aina zote za ndege wote. Mungu akaona kuwa ni vyema.

22. Mungu akavibariki, akasema, “Zaeni, muongezeke, muyajaze maji ya bahari; nao ndege waongezeke katika nchi.”

23. Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya tano.

24. Mungu akasema, “Nchi na itoe aina zote za viumbe hai, wanyama wa kufugwa, viumbe vitambaavyo na wanyama wa porini wa kila aina.” Ikawa hivyo.

25. Basi, Mungu akafanya aina zote za wanyama wa porini, wanyama wa kufugwa, na viumbe vitambaavyo. Mungu akaona kuwa ni vyema.

26. Kisha Mungu akasema, “Tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; atawale samaki wa baharini, ndege wa angani, wanyama wa kufugwa, dunia yote na viumbe vyote vitambaavyo.”

27. Basi, Mungu akaumba mtu kwa mfano wake; naam, kwa mfano wake Mungu alimuumba. Aliwaumba mwanamume na mwanamke.

28. Mungu akawabariki na kuwaambia, “Zaeni muongezeke, mkaijaze nchi na kuimiliki; muwatawale samaki wa baharini, ndege wa angani, na kila kiumbe hai kitembeacho duniani.”

29. Kisha Mungu akasema, “Tazama, nawapeni kila mmea duniani uzaao mbegu, na kila mti uzaao matunda yenye mbegu; mbegu zao au matunda yao yatakuwa chakula chenu.

30. Nao wanyama wote duniani, ndege wote wa angani, viumbe vyote vitambaavyo, naam, kila kiumbe chenye uhai, chakula chao kitakuwa majani yote ya mimea.” Ikawa hivyo.

31. Mungu akaona kila kitu alichokifanya kuwa ni chema kabisa. Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya sita.

Kusoma sura kamili Mwanzo 1