Agano la Kale

Agano Jipya

Mhubiri 2:13-24 Biblia Habari Njema (BHN)

13. Basi, mimi nikagundua kwamba hekima ni bora kuliko upumbavu, kama mwanga ulivyo bora kuliko giza.

14. Mwenye hekima anayo macho, huona aendako, lakini mpumbavu hutembea gizani. Hata hivyo, nikatambua kwamba mwenye hekima na mpumbavu mwisho wao ni uleule.

15. Basi, nikasema moyoni mwangu, “Yatakayompata mpumbavu yatanipata na mimi pia. Kwa nini, basi, nimekuwa na hekima kiasi chote hiki?” Nikajibu, nikiwaza, “Hayo nayo ni bure kabisa.”

16. Maana hakuna amkumbukaye mwenye hekima, wala amkumbukaye mpumbavu, kwani siku zijazo wote watasahaulika. Jinsi mwenye hekima afavyo ndivyo afavyo mpumbavu!

17. Kwa hiyo, nikayachukia maisha, maana yote yatendekayo duniani yalinisikitisha. Yote yalikuwa bure kabisa; nilikuwa nikifukuza upepo.

18. Nilichukia kazi yangu yote niliyokuwa nimefanya hapa duniani, kuona kwamba ilinipasa nimwachie mtu ambaye atatawala baada yangu.

19. Tena, ni nani ajuaye kwamba atakuwa mwenye hekima au atakuwa mpumbavu? Hata hivyo, yeye atamiliki yote niliyofanya kwa kutumia hekima yangu hapa duniani. Pia hayo yote ni bure kabisa.

20. Basi, nilipofikiria tena juu ya yote niliyofanya duniani, nilikata tamaa.

21. Maana, wakati mwingine mtu ambaye amefanya kazi kwa kutumia hekima, akili na maarifa yake, humwachia mtu mwingine afurahie matunda ya kazi ambayo hakuitolea jasho. Pia hilo nalo ni bure kabisa; ni jambo baya sana.

22. Mtu anafaidi nini kutokana na kazi zake zote, na juhudi anazohangaika nazo duniani?

23. Kwa sababu maisha yake yote yamejaa taabu, na kazi yake ni mahangaiko matupu; hata usiku akili yake haipumziki! Hayo nayo ni bure kabisa.

24. Hakuna chema kimfaacho binadamu, isipokuwa kula na kunywa na kuifurahia kazi yake. Hili nalo nimeliona kuwa latoka kwa Mungu,

Kusoma sura kamili Mhubiri 2