1. Mwanangu, usiyasahau mafundisho yangu,bali kwa moyo wako uzishike amri zangu.
2. Maana yatakupa wingi wa siku,maisha marefu na fanaka kwa wingi.
3. Utii na uaminifu visitengane nawe.Vifunge shingoni mwako;viandike moyoni mwako.
4. Hivyo utakubalika na kusifika,mbele ya Mungu na mbele ya wanadamu.
5. Mtumaini Mwenyezi-Mungu kwa moyo wako wote,wala usitegemee akili zako mwenyewe.
6. Umtambue Mungu katika kila ufanyalo,naye atazinyosha njia zako.
7. Usijione wewe mwenyewe kuwa mwenye hekima;mche Mwenyezi-Mungu na kujiepusha na uovu.
8. Hiyo itakuwa dawa mwilini mwako,na kiburudisho mifupani mwako.
9. Mheshimu Mwenyezi-Mungu kwa mali yako,na kwa malimbuko ya mazao yako yote.
10. Hapo ghala zako zitajaa nafaka,na mapipa yako yatafurika divai mpya.