Agano la Kale

Agano Jipya

Methali 2:3-19 Biblia Habari Njema (BHN)

3. naam, ukiomba upewe busara,ukisihi upewe ufahamu;

4. ukiitafuta hekima kama fedha,na kuitaka kama hazina iliyofichika;

5. hapo utaelewa ni nini kumcha Mwenyezi-Mungu,utafahamu maana ya kumjua Mungu.

6. Maana Mwenyezi-Mungu huwapa watu hekima;kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu.

7. Huwawekea wanyofu akiba ya hekima safi,yeye ni ngao kwa watu waishio kwa uaminifu.

8. Huilinda mienendo ya watu watendao haki,na kuzihifadhi njia za waaminifu wake.

9. Ukinisikiliza utafahamu uadilifu na haki,utajua jambo lililo sawa na jema.

10. Maana hekima itaingia moyoni mwako,na maarifa yataipendeza nafsi yako.

11. Busara itakulinda,ufahamu utakuhifadhi;

12. vitakuepusha na njia ya uovu,na watu wa maneno mapotovu;

13. watu waziachao njia nyofu,ili kuziendea njia za giza;

14. watu wafurahiao kutenda maovu,na kupendezwa na upotovu wa maovu;

15. watu ambao mienendo yao imepotoka,nazo njia zao haziaminiki.

16. Hekima itakuwezesha kumkwepa mwanamke mwasherati,mwanamke malaya wa maneno matamu;

17. mwanamke amwachaye mwenzi wa ujana wake,na kulisahau agano la Mungu wake.

18. Nyumba yake yaelekea kuzimu,njia zake zinakwenda ahera.

19. Yeyote amwendeaye kamwe harudi,wala hairudii tena njia ya uhai.

Kusoma sura kamili Methali 2