Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 9:10-24 Biblia Habari Njema (BHN)

10. Basi, wakachukua majivu kutoka kwenye tanuri, wakamwendea Farao, naye Mose akayarusha juu hewani.

11. Watu na wanyama wakavamiwa na majipu hata wale wachawi hawakuweza kujitokeza maana wao pamoja na Wamisri wote pia walivamiwa na majipu hayo.

12. Lakini Mwenyezi-Mungu akamfanya Farao kuwa mkaidi, naye hakuwasikiliza kama vile Mwenyezi-Mungu alivyomwambia Mose.

13. Kisha, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Kesho, amka alfajiri na mapema umwendee Farao, umwambie kwamba mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Waebrania, nasema hivi, ‘Waache watu wangu waondoke ili wakanitumikie.

14. Maana safari hii, wewe mwenyewe, maofisa wako na watu wako mtakumbana na mapigo yangu makali. Nawe utatambua kwamba hakuna yeyote duniani aliye kama mimi.

15. Ningalikwisha kukuangamiza tayari wewe na watu wako kwa maradhi mabaya, nanyi mngalikuwa mmekwisha angamia.

16. Lakini nimewaacheni muishi ili kudhihirisha uwezo wangu. Kwa hiyo dunia yote itatambua kuwa mimi ni nani.

17. Lakini bado unaonesha kiburi dhidi ya watu wangu, wala huwaachi waondoke.

18. Kwa hiyo kesho, wakati kama huu, nitaleta mvua kubwa ya mawe ambayo haijawahi kutokea nchini Misri, tangu mwanzo wake hadi leo.

19. Kwa hiyo agiza mifugo yako na chochote kilicho huko mashambani viwekwe mahali salama; kwa maana mvua ya mawe itamnyeshea kila mtu na mnyama aliye shambani na ambaye hayuko nyumbani; wote watakufa.’”

20. Baadhi ya maofisa wa Farao waliyatia maanani maneno hayo ya Mwenyezi-Mungu, wakawapeleka watumwa na wanyama wao nyumbani mahali pa usalama.

21. Lakini yule ambaye hakulijali neno la Mwenyezi-Mungu aliwaacha watumwa wake na wanyama wake mashambani.

22. Kisha, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nyosha mkono wako juu mbinguni, ili mvua ya mawe inyeshe kila mahali nchini Misri. Imnyeshee mtu, mnyama na kila mmea shambani.”

23. Basi, Mose alinyosha fimbo yake kuelekea mbinguni. Naye Mwenyezi-Mungu akaleta mvua ya mawe na ngurumo; umeme ukaipiga nchi. Mwenyezi-Mungu alinyesha mvua ya mawe nchini Misri,

24. mvua kubwa ya mawe iliyoandamana na mfululizo wa umeme, ambayo hakuna mwananchi yeyote wa Misri aliyepata kamwe kushuhudia kabla.

Kusoma sura kamili Kutoka 9