Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 9:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nenda kwa Farao ukamwambie kwamba mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Waebrania, nasema, ‘Waache watu wangu waondoke ili wakanitumikie.

2. Kama ukikataa kuwaacha waondoke na ukiendelea kuwashikilia,

3. nitaunyosha mkono wangu na kuleta maradhi mabaya sana juu ya mifugo yenu yote: Ng'ombe, farasi, punda, ngamia, mbuzi na kondoo.

4. Na, nitaitenganisha mifugo ya Waisraeli na mifugo ya Wamisri ili mnyama hata mmoja wa Waisraeli asife.’”

5. Tena, Mwenyezi-Mungu akaweka wakati maalumu akisema, “Kesho mimi Mwenyezi-Mungu nitatekeleza jambo hilo nchini Misri.”

6. Kesho yake Mwenyezi-Mungu akafanya alichosema. Mifugo yote ya Wamisri ikafa, lakini hakuna mnyama hata mmoja wa Waisraeli aliyekufa.

7. Farao akauliza habari juu ya wanyama wa Waisraeli, akaambiwa kuwa hakuna mnyama wao hata mmoja aliyekufa. Hata hivyo, Farao akabaki mkaidi, wala hakuwaruhusu Waisraeli waondoke.

8. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose na Aroni, “Chukueni kila mmoja wenu magao ya majivu ya tanuri, kisha Mose ayarushe juu hewani mbele ya Farao.

9. Majivu hayo yatakuwa vumbi nyembamba itakayoenea juu ya nchi yote ya Misri. Yatasababisha majipu yatakayotumbuka na kuwa vidonda kwa watu na wanyama kila mahali nchini Misri.”

10. Basi, wakachukua majivu kutoka kwenye tanuri, wakamwendea Farao, naye Mose akayarusha juu hewani.

11. Watu na wanyama wakavamiwa na majipu hata wale wachawi hawakuweza kujitokeza maana wao pamoja na Wamisri wote pia walivamiwa na majipu hayo.

Kusoma sura kamili Kutoka 9