Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 8:5-21 Biblia Habari Njema (BHN)

5. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mwambie Aroni anyoshe mkono wake na fimbo yake juu ya mito, juu ya mifereji na madimbwi, nao vyura watatokea na kuenea kila mahali nchini Misri.”

6. Basi, Aroni akanyosha fimbo yake juu ya maji yote, vyura wakatokea na kuifunika nchi nzima ya Misri.

7. Lakini wachawi wa Misri kwa uchawi wao pia wakaleta vyura nchini Misri.

8. Kisha Farao akamwita Mose na Aroni, akamwambia, “Msihi Mwenyezi-Mungu, ili aniondolee mimi na watu wangu vyura hawa, nami nitawaacha Waisraeli waende zao na kumtambikia Mwenyezi-Mungu.”

9. Mose akamjibu Farao, “Haya! Waweza kutaja wakati unaotaka nikuombee kwa Mungu, niwaombee maofisa wako na watu wako; nitamwomba awaangamize vyura hawa waliomo katika nyumba zenu; watabaki tu mtoni Nili!”

10. Farao akamwambia, “Kesho.” Mose akasema, “Nitafanya kama unavyosema, ili ujue kwamba hakuna yeyote anayelingana na Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.

11. Vyura wataondoka kwako, na kwenye nyumba zenu, kwa maofisa wako na kwa watu wako; watabaki tu katika mto Nili.”

12. Basi, Mose na Aroni wakaondoka nyumbani kwa Farao, na Mose akamlilia Mwenyezi-Mungu amwondolee Farao uvamizi wa vyura hao aliomletea.

13. Mwenyezi-Mungu akafanya kama Mose alivyomwomba: Vyura wakafa majumbani, viwanjani na kwenye kumbi za nyumba na katika mashamba.

14. Watu wakawakusanya vyura hao marundo marundo; nchi nzima ikanuka.

15. Lakini Farao alipoona kwamba nchi imepata nafuu, akawa mkaidi tena, wala hakuwasikiliza Mose na Aroni, kama Mwenyezi-Mungu alivyokuwa amesema.

16. Kisha, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mwambie Aroni anyoshe fimbo yake na kuyapiga mavumbi, nayo yatageuka kuwa viroboto kote nchini Misri.”

17. Mose na Aroni wakafanya hivyo. Aroni alinyosha fimbo yake na kuyapiga mavumbi, nayo yakageuka kuwa viroboto na kuwaparamia watu na wanyama. Mavumbi yote nchini kote Misri yakageuka kuwa viroboto.

18. Wachawi wa Misri, kwa uchawi wao, wakajaribu kuyageuza mavumbi yawe viroboto, lakini hawakufaulu. Viroboto hao wakaenea juu ya watu na wanyama.

19. Wale wachawi wakamwambia Farao, “Hii ni kazi ya mkono wa Mungu.” Lakini moyo wa Farao ukaendelea kuwa mgumu; wala hakuwasikiliza Mose na Aroni. Ikawa kama Mwenyezi-Mungu alivyokuwa amesema.

20. Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Kesho amka asubuhi mapema umwendee Farao wakati anapokwenda mtoni umwambie, ‘Mwenyezi-Mungu asema hivi: Waache watu wangu waondoke ili wanitumikie.

21. Kama ukikataa kuwaacha waondoke, basi, nitakuletea makundi ya nzi, wewe, maofisa wako na watu wako wote. Wataingia kwenye nyumba zenu na nyumba zote za Wamisri zitajaa makundi ya nzi, kadhalika na ardhi yote ya Misri.

Kusoma sura kamili Kutoka 8